Home » » MAKALA MAALUMU : Njaa Katavi: Ni umasikini au soko huria?

MAKALA MAALUMU : Njaa Katavi: Ni umasikini au soko huria?




Na Walter Mguluchuma
KWA wakazi wa mikoa ya Rukwa na Katavi ni masikini ni miongoni mwa kauli ambazo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya amekuwa akiipinga na kuwaomba waandishi wa habari kuacha kuitumia.
Rukwa ni mkoa dada wa Katavi na wakati huo Manyanya akizungumza kuwa wakazi wa Rukwa si masikini, alikuwa akiwazungumzia pia wakazi wa wilaya ya Mpanda kwani wilaya hiyo inayounda mkoa wa Katavi, ilikuwa sehemu ya mkoa wa Rukwa.
“Unaposema wakazi hawa ni masikini, kwanza unakuwa huwatendei haki kwani hawajawahi kukosa chakula cha siku hata mara moja. Hizo ni kauli za kukatisha tamaa ambazo mara kwa mara hutolewa na viongozi wa upinzani,” aliwahi kunukuliwa akisema mama huyo.
Lakini hata mwaka haujakwisha tangu atoe kauli hiyo, tayari kuna kila dalili za njaa kuikumba mikoa hiyo ambayo ni miongoni mwa mikoa inayozalisha kwa wing mazao ya chakula, hasa mahindi.
Vyombo vya habari vimeanza kuripoti na hata hali halisi hapa mjini Mpanda inaonyesha kuwa hofu ya njaa miongoni mwa wananchi inaongezeka kila siku.
Injinia Manyanya alisema wananchi wake hawajawahi kukosa chakula cha siku, lakini ukweli kwa sasa, kwa mujibu wa utafiti wa mwandishi wa makala haya, wananchi wa wilaya za Mpanda na Mlele mkoani Katavi, wameanza kula mlo mmoja tu kwa siku.
Hali hii inatokana na kutokana kwa bei ya nafaka, hasa mahindi ambayo ni chakula kikuu kwa jamii ya hapa, tofauti na miaka mingine.
Kwa kawaida bei ya mahindi na nafaka nyingine huwa ni ya kuridhisha kwa miezi hii huku kila familia ikiimudu kwani ni miezi michache tangu kumalizika kwa msimu wa mavuno.
Kipindi cha mavuno kwa Mpanda ni kuanzia Machi hadi Juni, wakati Sumbawanga huwa ni Mei hadi Julai; na wakati huo bei ya mahindi hushuka sana.
“Mwanzoni mwa mwezi huu (Oktoba) bei ya debe moja la mahindi ilikuwa ni Sh 8,000 na kufikia katikati ya mwezi, debe hilo limefika Sh 12,000,” mkazi mmoja wa Mpanda anasema.
Debe ndio kipimo cha ununuzi wa mazao mkoani hapa, na aghalabu debe moja huwa sawa na kilo 20 za mahindi, kwa kurahisisha, kwa sasa kilo moja ya mahindi ambayo hayajakobolewa ni Sh 600, bei ambayo ni kubwa sana kwa watu wa maisha ya kati.
Lakini ni kwanini bei imefika hapo?
“Tatizo ni kwamba wakulima wengi, kutokana na umasikini au hali ngumu ya maisha, wameuza chakula chote walichokivuna kwa wafanyabiashara wanaopeleka mazao nje ya mkoa na hata nje ya nchi,” anasema mkazi mwingine.
Wakulima, kwa tamaa ya fedha, wameuza na wanaendelea kuuza mazao kwa wafanyabiashara ambao wengine huja na kuyauza mjini kwa bei kubwa. Ikumbukwe wakulima hawa wanaachwa bila akiba na sia jabu mwakani serikali ikalazimika kuleta msaada wa chakula.
“Mara nyingi chakula hufikia bei ya kutisha kama ya sasa kwenye miezi ya Januari na Februari. Wakati huo wengi huwa wamemaliza akiba walizojiwekea. Lakini iwapo bei hizo ndizo zipo Oktoba, itakuwaje Februari mwakani?” anahoji mfuatiliani mwingine wa hali ya mambo wilayano hapa.
Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Kanali Ngemela Lubinga alieleza kushitushwa na kitendo cha wananchi wake kuuza kwa kasi mahindi wakati huu wa kiangazi, huku kukiwa na ‘uvamizi’ wa walanguzi kutoka mikoa ya Shinyanga, Mwanza na Mara.
Mwenzake wa Wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima, alisema bei ya mahindi inapopanda, anayefurahia na kufaidika na hali hiyo ni muuzaji (mfanyabiashara) na wala si mlaji.
Wengi wametoa wito kwa serikali kuwaelimisha wakulima kuwa na tabia ya kujiwekea akiba ya chakula kwani hali itakapokuwa mbaya, ni serikali hiyo hiyo ndiyo italazimika kuwatumia chakula cha msaada.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Katavi yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa