Na Walter Mguluchuma
KWA wakazi wa mikoa ya Rukwa na Katavi ni
masikini ni miongoni mwa kauli ambazo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella
Manyanya amekuwa akiipinga na kuwaomba waandishi wa habari kuacha kuitumia.
Rukwa ni mkoa dada wa Katavi na wakati huo
Manyanya akizungumza kuwa wakazi wa Rukwa si masikini, alikuwa akiwazungumzia
pia wakazi wa wilaya ya Mpanda kwani wilaya hiyo inayounda mkoa wa Katavi,
ilikuwa sehemu ya mkoa wa Rukwa.
“Unaposema wakazi hawa ni masikini, kwanza
unakuwa huwatendei haki kwani hawajawahi kukosa chakula cha siku hata mara
moja. Hizo ni kauli za kukatisha tamaa ambazo mara kwa mara hutolewa na
viongozi wa upinzani,” aliwahi kunukuliwa akisema mama huyo.
Lakini hata mwaka haujakwisha tangu atoe
kauli hiyo, tayari kuna kila dalili za njaa kuikumba mikoa hiyo ambayo ni
miongoni mwa mikoa inayozalisha kwa wing mazao ya chakula, hasa mahindi.
Vyombo vya habari vimeanza kuripoti na hata
hali halisi hapa mjini Mpanda inaonyesha kuwa hofu ya njaa miongoni mwa
wananchi inaongezeka kila siku.
Injinia Manyanya alisema wananchi wake
hawajawahi kukosa chakula cha siku, lakini ukweli kwa sasa, kwa mujibu wa
utafiti wa mwandishi wa makala haya, wananchi wa wilaya za Mpanda na Mlele
mkoani Katavi, wameanza kula mlo mmoja tu kwa siku.
Hali hii inatokana na kutokana kwa bei ya
nafaka, hasa mahindi ambayo ni chakula kikuu kwa jamii ya hapa, tofauti na
miaka mingine.
Kwa kawaida bei ya mahindi na nafaka
nyingine huwa ni ya kuridhisha kwa miezi hii huku kila familia ikiimudu kwani
ni miezi michache tangu kumalizika kwa msimu wa mavuno.
Kipindi cha mavuno kwa Mpanda ni kuanzia
Machi hadi Juni, wakati Sumbawanga huwa ni Mei hadi Julai; na wakati huo bei ya
mahindi hushuka sana.
“Mwanzoni mwa mwezi huu (Oktoba) bei ya
debe moja la mahindi ilikuwa ni Sh 8,000 na kufikia katikati ya mwezi, debe
hilo limefika Sh 12,000,” mkazi mmoja wa Mpanda anasema.
Debe ndio kipimo cha ununuzi wa mazao
mkoani hapa, na aghalabu debe moja huwa sawa na kilo 20 za mahindi, kwa kurahisisha,
kwa sasa kilo moja ya mahindi ambayo hayajakobolewa ni Sh 600, bei ambayo ni
kubwa sana kwa watu wa maisha ya kati.
Lakini ni kwanini bei imefika hapo?
“Tatizo ni kwamba wakulima wengi, kutokana
na umasikini au hali ngumu ya maisha, wameuza chakula chote walichokivuna kwa
wafanyabiashara wanaopeleka mazao nje ya mkoa na hata nje ya nchi,” anasema
mkazi mwingine.
Wakulima, kwa tamaa ya fedha, wameuza na
wanaendelea kuuza mazao kwa wafanyabiashara ambao wengine huja na kuyauza mjini
kwa bei kubwa. Ikumbukwe wakulima hawa wanaachwa bila akiba na sia jabu mwakani
serikali ikalazimika kuleta msaada wa chakula.
“Mara nyingi chakula hufikia bei ya kutisha
kama ya sasa kwenye miezi ya Januari na Februari. Wakati huo wengi huwa
wamemaliza akiba walizojiwekea. Lakini iwapo bei hizo ndizo zipo Oktoba,
itakuwaje Februari mwakani?” anahoji mfuatiliani mwingine wa hali ya mambo
wilayano hapa.
Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Kanali Ngemela
Lubinga alieleza kushitushwa na kitendo cha wananchi wake kuuza kwa kasi
mahindi wakati huu wa kiangazi, huku kukiwa na ‘uvamizi’ wa walanguzi kutoka
mikoa ya Shinyanga, Mwanza na Mara.
Mwenzake wa Wilaya ya Mpanda, Paza
Mwamlima, alisema bei ya mahindi inapopanda, anayefurahia na kufaidika na hali
hiyo ni muuzaji (mfanyabiashara) na wala si mlaji.
Wengi wametoa wito kwa serikali
kuwaelimisha wakulima kuwa na tabia ya kujiwekea akiba ya chakula kwani hali
itakapokuwa mbaya, ni serikali hiyo hiyo ndiyo italazimika kuwatumia chakula
cha msaada.
No comments:
Post a Comment