Na Walter Mguluchuma .
Katavi .
Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Katavi kimetengua matokeo ya uchaguzi kwa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Tanganyika na nafasi ya Katibu wa siasa na uenezi pamoja na wajumbe wa kamati ya siasa ya Wilaya ambapo Yasin Kibiriti alikuwa ameisha tangazwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Wilaya hiyo baada ya kubainika msimamizi wa uchaguzi alikiika kanuni za uchaguzi .
Uamuzi wa kufuta matokeo hayo ya uchaguzi ulitolewa hapo jana na kikao maalumu cha kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa Katavi kilichofanyika katika ukumbi wa idara ya Maji kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Ccm Mkoa wa Katavi Mselemu Abdallah.
Katibu wa Ccm wa Mkoa wa Katavi Kajoro Vyohoroka aliwaambia wandishi wa Habari jana ofisini kwake kuwa kikao hicho kilipokea malalamiko ya uchaguzi wa CCM Wilaya ya Tanganyika kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Wilaya ambapo uchaguzi wake ulifanyika terehe 10 oktoba na Yasin Kiberiti alitangazwa na msimamizi mkuu wa uchaguzi huo kuwa ndiye mshindi.
Alisema kikao hicho kilbaini kuwa ni kweli kwenye uchaguzi huo kanuni ya uchaguzi ilikiukwa na msimamizi mkuu wa uchaguzi Crisant Mwanawima ambae alikiuka kanuni ya uchaguzi ya mwaka 2012 ibara ya 11b.
Aidha ibara ya 21 b ya kanuni inaeleza wazi kwamba mshindi katika uchaguzi kwa wagombea wasio kundini lazima mshindi atakae tangazwa awe amevuka zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa .
Kajoro alifafanua kuwa kwa matokeo yaliotangazwa siku hiyo ya msimamizi mkuu wa uchaguzi yalikuwa yafuatayo kura zilizopigwa zilikuwa 458 kura halali 450 na kura zilizoharibika 8 ambapo Yasin Kiberiti alipata kura 222 Abdallah Sumry kura 176 na Mombo Rashid Mombo kura 55.
Alisema kwa mantiki hiyo kikao kiliamua kutegua matokeo yote ya uchaguzi wa CCM wa Wilaya ya Tanganyika kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Ccm Wilaya ,Katibu wa siasa na uenezi wa Wilaya na wajumbe wote wa kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya Ccm Wilaya.
Katibu huyo wa CCM wa Mkoa alizitaja sababu zilizopelekea kutengua kwa matokeo ya mshindi wa Mwenyekiti wa ccm wa Wilaya kuwa ni mshindi kwenye uchaguzi huo hakupata zaidi ya nusu ya kura halali zilizopingwa kwa mujibu wa kanuni ya uchaguzi .
Kwani Kikao kilichotengua matokeo hayo kilibaini kuwa msimamizi mkuu wa uchaguzi kabla ya kutangaza matokeo hayo yawezekana alifanya kwa makusudi kwa lengo la kumbeba mgombea mmoja na ndio maana hakumshirikisha msimamizi msaidizi wa uchaguzi wala mkurugenzi wa uchaguzi wa wilaya hiyo.
Alisema kwakuwa Mwenyekiti alitangazwa mshindi kinyume na kanuni za uchaguzi ndani ya chama hivyo hivyo hata kikao cha Halmashauri kuu ya Ccm alichokiongoza baada ya kuchaguliwa nacho kilikuwa ni batili hivyo matokeo ya Katibu na uenezi pamoja na wajumbe wa kamati ya siasa ya Wilaya nao uchaguzi wao umefutwa.
Kuhusu adhabu aliyopewa msimamizi huyo wa uchaguzi Kajolo alisema amepewa adhabu kwa mujibu wa kanuni za chama za uongozi na maadili kwa kushindwa kwake kusimamia vema uchaguzi huo huku akiwa anajua kuwa anavunja kanuni ya uchaguzi.
mwisho
0 comments:
Post a Comment