Home » » WIZARA ZINAZOLIMBIKIZA MADENI ZIWAJIBISHWE

WIZARA ZINAZOLIMBIKIZA MADENI ZIWAJIBISHWE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Tumeridhishwa na juhudi zinazofanywa na Wizara ya Fedha hivi sasa katika kuhakikisha inakuwapo nidhamu katika matumizi ya fedha katika wizara za Serikali. Tunashuhudia sasa jinsi wizara hiyo inavyopambana na vitendo vya wizi na ubadhirifu wa fedha za Serikali. Tunaweza kusema, pasipo kutafuna maneno, kwamba sasa vita dhidi ya ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma ni ya dhati tofauti na huko nyuma ambako vita hiyo ilikuwa ikiendeshwa kisiasa. Kwa mara ya kwanza, Wizara ya Fedha iko mstari wa mbele katika vita hiyo na mafanikio sasa yameanza kupatikana.
Matokeo ya kazi nzuri inayosimamiwa na uongozi mpya wa Wizara ya Fedha yametuthibitishia, pasipo kuacha shaka, kwamba wizi na ubadhirifu wa fedha za Serikali unafanywa na watumishi ndani ya Serikali, ikiwa ni pamoja na watumishi wa Wizara ya Fedha. Mwelekeo mpya wa wizara hiyo sasa umewezesha kuokolewa kwa fedha nyingi za Serikali zilizokuwa zikiibwa kupitia njia mbalimbali, ikiwamo mishahara hewa. Wizara ya Fedha imesema udhibiti wa mishahara hewa pekee unaokoa Sh40 bilioni kwa mwezi.
Hayo ni mafanikio makubwa. Wizara hiyo sasa imepanua wigo katika udhibiti wa fedha za Serikali. Baada ya kugundua kuwa wizara zinadaiwa madeni makubwa, ingawa fedha zinatengwa kila mwaka kulipia madeni hayo, Wizara ya Fedha imeingilia kati kwa kuamua kukata fedha moja kwa moja kutoka kwenye mafungu yaliyopangwa kutolewa kwa mwaka huu wa fedha. Wizara imebaini kwamba madeni mengi katika baadhi ya wizara yanatokana na kutumia fedha zilizotengwa kulipia matumizi fulani, kutumika kwa matumizi mengine kinyume na taratibu na kanuni za fedha za Serikali.
Ni hivi karibuni tu ofisi ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), iliamua kuwatimua baadhi ya wapangaji wa nyumba zake zilizopo mjini Dodoma ambao ni wadaiwa sugu, wakiwamo mawaziri saba na kukabidhi majina yao kwa kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart ili iwaondoe kwa nguvu katika nyumba hizo. Kwa maana hiyo, fedha za kulipia pango la mawaziri hao zilitengwa katika bajeti, lakini zilielekezwa kwenye matumizi mengine. Wizara hiyo sasa imeamua kukata fedha za deni hilo moja kwa moja kutoka kwenye mafungu yaliyopangwa kwa mwaka huu wa fedha na imesema hatua hiyo itahusu pia madeni mengine kama ya umeme, maji, mawasiliano na kadhalika.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Katavi yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa