Home » » FANYENI TAFITI ZA MAZAO YA KILIMO

FANYENI TAFITI ZA MAZAO YA KILIMO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 

WATAALAMU wa tafiti za mazao ya kilimo na chakula nchini wameshauriwa kuendelea kufanya tafizi za mazao mbalimbali ili kusaidia upatikanaji wa mbegu bora lengo likiwa ni kumkomboa mkulima aweze kupata mavuno mengi.

Ushauri huo umetolewa na mkimbiza mwenge wa uhuru kitaifa Hamza Mahamud mara baada ya kukagua shamba la mfano lenye ukubwa wa ekari tatu za muhogo aina ya kiroba lililopo kwenye kijiji cha Gombero wilayani Mkinga hapo jana.

Alisema kuwa mbegu hiyo licha ya kuwa ya majaribio lakini tayari imeanza kuonyesha matokeo bora katika maeneo mbalimbali ilipopandwa hali inayotoa matumaini kuwa aina hiyo ya mbegu ni mkombozi wa mkulima wa muhogo hapa nchini.

"Nawahimiza wakulima wote nchini endeleeni kulima kilimo chenye tija kwa kuhakikisha mnapata mbegu bora, pembejeo bora pamoja na kupanda kwa wakati huku mkifuatilia kwa ukaribu ushauri wa wataalamu wetu,"alisema Mahamud.

Vile vile aliwaomba wataalamu hao kuhakikisha wanapata tiba ya magonjwa ya mazao hayo pamoja na kuwashauri wakulima njia bora za kilimo kwa lengo la kumkomboa mkulima hasa wa kijijini kwani maisha yao yote yanategemea kilimo.

Nae msimamizi wa shamba hilo Lucy Yohana alisema kuwa shamba la mfano hilo limeweza kutumia kiasi cha sh. milioni 2.6 toka maandalizi ya shamba hadi palizi nne ambapo wanatarajia kupata mbegu milioni 49 baada ya mavuno ya kwanza ambazo zitaweza kusambazwa kwa wakulima wilayani humo.

Hata hivyo alisema kuwa changamoto kubwa wanayoipata sasa ni mbegu hiyo kuanza kushambuliwa na ugonjwa wa batobato hali ambayo imesababisha kuharibu zao hilo, kwa kipindi cha miezi mitano zaidi ya mashina 40 mpaka sasa yameharibika toka kupandwa.

Jambo jingine lililozungumzwa na Mahamud ni kuwaomba Watanzania kuendelea kuitunza tunu ya amani iliyopo nchini

Chanzo:Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Katavi yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa