Home » » VIONGOZI WATANO WA CHAMA CHA WALIMU WATIWA MBARONI MPANDA

VIONGOZI WATANO WA CHAMA CHA WALIMU WATIWA MBARONI MPANDA



Na, Walter Mguluchuma, Mpanda – Katavi yetu blog

Jeshi la  Polisi Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi linawashikilia viongozi watano wa chama cha Walimu Wilaya ya Mpanda kwa kudaiwa kuhamasisha mgomo wa waalimu.

Viongozi hao walikamatwa na Polisi hapo jana majira ya saa kumi na mbili jioni wakati wakizunguka katika mitaa mbalimbali ya Mji wa Mpanda wakiwatangazia walimu kuwa kuanzia Juma tatu Julai 30 kutakuwa na mgomo rasmi wa walimu Nchi nzima.

Viongozi waliokamatwa ni Izack Malilo Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Mpanda na Katibu wake Nicodemas Waivyala.

Wengine Mhasibu wa Chama hicho Emmanuel Kabale Asha Juma Mjumbe wa Kitengo cha walimu wanawake na Paulo Guyashi.

Kwa upande wake Mjumbe wa kamati tendaji ya CWT Wilaya hiyo Njiku Ramadhani alilalamikia Jeshi la Polisi kwa kitendo cha kuwakamata na kuwaweka ndani Viongozi hao.

Alisema Mgomo huo wa walimu upo kihalali Nchi nzima na siyo Mpanda pekee yake na pia ni wajibu wao Viongozi wa Chama Cha Walimu kufanya walivyo fanya kwani ni jukumu lao kutekeleza maagizo yanayotolewa na viongozi wao wa juu wa CWT.

Njiku aliendelea kueleza ingekuwa mgomo huo wa waalimu sio halali basi viongozi wao wa ngazi ya Taifa nao pia wangekamatwa.

Mwandishi wa habari hizi aliyetembelea shule mbalimbali za Mji wa Mpanda alishuhudia wanafunzi wakiwa wanacheza nje tuu kutokana na walimu kutoingia madarasani na wengine kutofika kabisa.

Baadhi ya waalimu ambao hawakufika kabisa Shuleni wamewalaumu waalimu wenzao kwa kudai kuwa ni waalimu ambao hawajiamini na ndiyo waalimu ambao hawana Vyeti.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Katavi dhahiri Kidavashari amethibitisha kukamatwa kwa viongozi hao na jeshi la polisi linaangazia namna ya kuwapa mdhamana muda wowote kuanzia sasa

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Katavi yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa