Mpanda.
Uongozi wa Chama cha Walimu (CWT) Mikoa ya Rukwa na Katavi wamelaani vikali hatua ya jeshi la polisi mkoani humo kuwakamata baadhi ya viongozi wa chama hicho na kwamba kitendo cha kuwatishia viongozi wa CWT ni kukiukwa kwa haki za binadamu.
Chama hicho kimesema kitendo hicho ni uonevu na kwamba wataendelea na mgomo wao licha Jeshi la polisi kuanza kuwatisha kwa kuwakamata baadhi ya viongozi wa chama hicho.
Tamko hilo la CWT limetolewa julai 30, mwaka huu kufuatia viongozi watano wa chama hicho wilayani Mpanda mkoani Katavi kukamatwa na jeshi la Polisi kwa madai ya kushiriki kuhamasisha mgomo kwa Walimu wa mkoa huo.
Katibu wa CWT mkoani Rukwa na Katavi Dweesdeur Zambi amesema kuwa mgomo wao uko kisheria hivyo kamwe hawatatishwa na vitisho vyovyote vitakavyofanywa na serikali kwa lengo la kutaka kuuzima mgomo huo.
Walimu hao wamelazimika kugoma kwa kufuata sheria namba 6 ya Ajira na Utumishi ya mwaka 2004 ambayo inawalinda Walimu hao kuingia katika mgomo pasipo kuingiliwa na chombo chochote cha dola.
Katibu huyo alisema tathimini ya awali ya mgomo huo Mkoani Rukwa na Katavi inaonesha kuwa Walimu wengi wameitikia mgomo huo na wanaendelea kupata mawasiliano ya kila wakati kutoka kwa viongozi wao wa wilaya.
Jumla ya viongozi watano wa CWT wanaoshikiliwa na jeshi la Polisi mkoani Katavi ni pamoja Mwenyekiti wa CWT wilayani Mpanda Bw.Isaack Martine, Katibu wake Bw.Nicodemus Waivyala na Mwakilishi wa Wanawake wa chama hicho wilayani Mpanda Asha Juma na Walimu wengine wawili.
Blogzamikoa
www.blogszamikoa.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment