Katibu Mtendaji wa Rango, Stanley Mshana, akitoa mdahalo wa kuhamasisha jamii kuhusu usawa wa kijinsia na haki ulioandaliwa na muungano wa asasi isiyo ya kiserikali mkoani Rukwa (Rango) kwa ufadhili wa The Foundation for Civil Society na kufanyika katika kata ya Stalike wilayani Mpanda.
Mussa Mwangoka-Katavi yetu.
KUSHAMIRI kwa mfumo dume katika wilaya ya Mpanda mkoani Katavi kunaathiri kwa kiasi kikubwa hali ya kiuchumi kwa wanawake ambao ndio nguvu kazi kubwa katika uzalishaji wa mazao yatokanayo na kilimo.
Baadhi ya wanawake wa Kata ya Stalike wilayani Mpanda walisema hayo jana wakati wakizungumza kwenye mdahalo wa kuhamasisha jamii kuhusu usawa wa kijinsia na haki ulioandaliwa na muungano wa asasi isiyo ya kiserikali mkoani Rukwa (Rango) kwa ufadhili wa The Foundation for Civil Society.
Mmoja wa wanawake hao, Mariam Iddy alisema kuwa wanawake ndio wamekuwa na mchango mkubwa katika uzalishaji mali kupitia kilimo lakini kipato kinachopatikana mara baada ya kuuza mazao waliyozalisha huishia mikononi mwa wanaume ambao hujikita kwenye vitendo vya starehe na kusahau malezi ya familia zao.
Alisema kuwa inapofika kipindi cha kuvuna mwanaume huanza kubadilika kwa kutafuta sababu mbali mbali za kuonyesha chuki ndani ya nyumba ili aweze kupata sababu za kuuza mazao pepe yake bila kumshirikisha mke wake.
“Hali hii inatusikitisha sana kwani akishauza mazao haya huondoka nyumbani na kwenda kufanya starehe zake na wanawake wengine , lakini baada ya fedha kuisha na hurudi nyumbani na kuanza kutafuta visababu vidogo vidogo ambavyo usababisha kutokea kwa mfarakano ndani ya familia” alisema
Aliongeza kuwa athari ambazo wanapata baada ya mfarakano ni kuachiwa familia na kupata shida katika kuihudumia ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto na mahitaji mengine ya nyumbani ambayo ni muhimu.
Naye, Beatrice John, alisema kufutia vitendo hivyo vya wanaume ni muhimu elimu ya usawa wa kijinsia ikatolewa mara kwa mara hasa maeneo ya vijijini ambako mifumo dume ndio inaonekana kutawala hali ambayo itasaidia kupunguza hali hiyo katika jamii.
“Tunaomba waume zetu waache tabia hii kwani mazao haya tunalima sote hivyo hata wakati wa kuvuna inatakiwa tuwe pamoja na hata kuuza vile vile inatakiwa kusimama kwa pamoja kama mke na mume ili fedha zitakapopatikana mazao na kuuza yaweze kusaidia kulea familia zetu pamoja na kusomesha”alisema Beatrice.
0 comments:
Post a Comment