*Ni katika shule yenye umri wa zaidi ya miaka 40
*Tatizo la maji ya kujisitiri msalani lazidisha kero
NA WALTER MGULUCHUMA, Katavi
Wakati
Bunge la Bajeti likiendelea na vikao vyake mjini Dodoma, wadau wa elimu
mkoani Katavi wameonekana kusikitishwa na uduni wa mazingira yaliyopo
katika shule mbalimbali mkoani hapa.
Katavi
ni miongoni mwa mikoa inayofanya vyema katika sekta ya elimu kwa miaka
ya karibuni, ikishika nafasi za juu katika matokeo ya jumla ya darasa la
saba na hata kidato cha nne.
Lakini
nyuma ya mafanikio hayo yanayodaiwa kupatikana kwa jasho la walimu
wenye uzalendo mkubwa na kitihada za wazazi na wanafunzi, shule nyingi
zimekuwa zikikabiliwa na mazingira duni katika kila hali.
Utafiti
uliofanywa na MWANDISHI WA HABARI HIZI uligundua kuwa moja kati ya
shule zenye changamoto zinazoweza kutatuliwa kwa ushirikishwaji kati ya
serikali na wadau ni Shule ya Msingi Mtapenda.
Shule
hiyo ipo katika Halmashauri ya Nsimbo, Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi,
ikiwa takriban kilomita 15 tu kutoka mkoani, lakini haina makazi ya
walimu na nyumba iliyopo inayotumiwa na Mwalimu Mkuu, haina hata choo.
Shule
hiyo ilianzishwa zaidi ya miaka 40 iliyopita wakati Serikali ya Awamu
ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ilipoendesha
Operesheni Vijiji.
Walimu
16 wanaofanya kazi shuleni hapo kwa sasa wote wanaishi katika nyumba za
kupanga, nyingi zikikosa hadhi ya kuishi mfanyakazi wa serikali na
hivyo wengine kuishi kijiji jirani, wakilazimika kusafiri mwendo mrefu
kufika kazini.
“Hata
hiyo nyumba anayoishi Mwalimu Mkuu nayo ni majanga tu. Haina choo! Kwa
hiyo mwalimu analazimika kuomba msaada kwa majirani kujisitiri. Ni aibu
kwa kweli,” anasema mmoja wa walimu wa shule hiyo aliyeomba hifadhi ya
jina lake.
Hata
hivyo, zipo nyumba (au tuseme mahame) zilizokuwa zimejengwa kwa ajili
ya walimu jirani na shule hiyo ambazo kwa hakika ni chakavu kiasi cha
kuonekana kama ‘makaburi’ kwa yeyote atakayejaribu kuzitumia, zikiwa
zimejengwa kwa udongo.
Mwalimu
mmoja aliyejitosa kuishi katika moja ya nyumba hizo anadai kuwa nyakati
za mvua huwa hakuna kulala kwani nyumba hizo zinavuja.
“Ni sawa na kukaa chini ya mwembe. Hapo utafurahia kivuli tu lakini mvua ikija, hapafai,” anasema mwalimu huyo.
Diwani
wa Mtapemba, Eliezer Fyula anakiri kulifahamu tatizo la uhaba wa nyumba
shuleni hapo, akidai kuwa lipo kwa muda mrefu sasa.
“Hapa
tuna bahati kwa kuwa tuna walimu 16, lakini ni bahati mbaya kwamba
nyumba zilizoandaliwa kwa ajili yao ni tano tu, nazo ni chakavu kama
unavyoziona.
“Ni
moja tu ndio imejengwa kwa matofali ya kuchoma, nyingine ni matofali ya
udongo tu. Wenyewe wanaita biskuti. Zipo katika hali mbaya sana,”
anasema Fyula.
Anasema
tatizo hilo linachagizwa na Halmashauri ya Nsimbo kutotenga fedha kwa
ajiri ya ujenzi wa nyumba za walimu licha ya yeye kuishauri mara kwa
mara.
Kwa
upande mwingine, katika Kijiji cha Majimoto wilayani Mlele, tatizo la
maji lililopo maeneo hayo husababisha hata wanafunzi kushindwa kuendelea
na ratiba ya masomo kama ilivyopangwa.
Katika
Shule ya Msingi Majimoto, MWANDISHI WA HABARI HIZI iliwashuhudia
watoto wakitoka madarasani kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi,
hasa ya chooni, kwani shule haina kisima wala bomba la maji.
Wakizungumza
na mwandishi wetu, wanafunzi hao waliokuwa wakichota maji katika
chemchem maarufu inayotoa maji ya moto, walilalamikia hali hiyo.
“Shuleni
hakuna huduma yoyote ya maji na kama kusingekuwapo chemchem hapa
karibu, sijui tungepata wapoi maji. Kila mara huwa tunakatisha masomo
kuja kuchota maji,” anasema mtoto mmoja wa darasa la tatu.
Ni
kawaida kwa kila mwanafunzi anayesoma shuleni hapo kuwa na dumu (kopo
la plastiki) la lita tano kwa ajili ya kuchotea maji kwenye chemchem
hiyo.
Jina
la kijiji, Majimoto, linatokana na kuwapo kwa chemchem hiyo inayotoa
maji ya moto kiasi cha kulazimika kuyapoozesha kabla ya kuyatumia. Maji
hayo hutiririka kwa mwaka mzima.
Hata hivyo, maji hayo yanayotokana na nguvu za asili (volcano), hayafai kwa kunywa.
“Tumeshazoea
kwa sababu imekuwa kawaida kabisa kuja kuchota maji hapa. Tutfanyaje na
chooni hakuna maji? Ni lazima kila sku kuja hapa kuchota maji,” anasema
binti huyo.
Pamoja
na kufahamu kwamba maji ya chemchem hiyo hayafai kwa kunywa, MWANDISHI
iliwashuhudia watoto kadhaa wakiyanywa baada ya kupoa, wakisema hawana
sehemu nyingine ya kupata maji ya kunywa.
Kwa
ujumla maji ni tatizo kubwa kijijini hapo na wananchi husafiri kwa
takriban kilomita sita kufuata maji katika Kijiji cha Mamba.
0 comments:
Post a Comment