Home » » SERIKALI YAZUIA UZALISHAJI HOLELA WA VITABU

SERIKALI YAZUIA UZALISHAJI HOLELA WA VITABU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesikia kilio cha muda mrefu juu ya uzalishaji wa vitabu usiokidhi viwango kwa kufuta mfumo huria wa uzalishaji na usambazaji wa vitabu shuleni na vyuo vya ualimu badala yake jukumu hilo sasa litafanywa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
Taasisi hiyo sasa itachapisha vitabu vya kiada na kuvisambaza kwa utaratibu wa kitabu kimoja kwa kila darasa na kila somo kwa ngazi za Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Mafunzo ya Ualimu.
Pia TET itaratibu maandalizi na uzalishaji vitabu vya ziada na vifaa vingine vya elimu kama vifaa vya kujifunzia na kufundishia, vitakavyoandaliwa na wachapaji binafsi.
Maagizo hayo yamo kwenye waraka mpya wa elimu namba 4 wa mwaka 2014 uliotolewa na wizara hiyo na kusainiwa na Kamishna wa Elimu, Profesa Eustella Bhalalusesa.
Waraka huo unafuta waraka namba 7 wa mwaka 2005 na unaanza kutumika Septemba Mosi, mwaka huu (leo).
Waraka huo mpya ndio unaoelekeza kuwa sera ya mfumo huria wa uzalishaji na usambazaji wa vitabu na vifaa vingine vya kielimu umefutwa rasmi.
Mfumo huo huria ulikuwa unaielekeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kujitoa katika uandishi wa vitabu na kuacha jukumu hilo kwa wachapishaji binafsi utaratibu ulioanzishwa mwaka 1991.
"Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mamlaka aliyonayo chini ya ‘Kifungu Na 54 cha Sheria ya Elimu Sura ya 353’ amefuta Sera ya Uzalishaji na Usambazaji wa Vitabu Shuleni na Vyuo vya Ualimu ya Mwaka 1991.
Kuwepo kwa mfumo huria wa uchapishaji na usambazaji wa vitabu ulilalamikiwa na wadau wengi wa elimu kuwa ulikuwa unaruhusu kuchapishwa kwa vitabu visivyo na ubora na kutumiwa na wanafunzi hali ambayo ilidumaza utoaji wa elimu nchini.
Mabadiliko hayo yanadhihirisha namna ambavyo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawamba amesikia kilio cha wadau wa elimu nchini.
Kabla ya kutoa waraka huo mpya unaoanza kutumika leo, Wizara hiyo inayosimamia ubora wa elimu nchini, ilitangaza pia kuvunjwa kwa iliyokuwa Kamati ya Ithibati ya Vifaa vya Kielimu (Emac) iliyoanzishwa mwaka 2005 ambayo ililalamikiwa kudidimiza elimu nchini.
Chini ya mfumo huo mpya utayarishaji wa vifaa vingine vya elimu vitakavyoandaliwa na watu binafsi, vitawasilishwa kwa Taasisi ya Elimu Tanzania kwa ajili ya uhakiki.
Chanzo;Habari Leo 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Katavi yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa