Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WADAU wa maendeleo mkoani Rukwa wametakiwa kuchangamkia fursa za
uwekezaji hususani katika sekta ya elimu ili iwe chachu ya kuongeza
wataalamu wa kada mbalimbali mkoani humo ambao watasaidia kupatikana kwa
maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM
mkoani Rukwa, Rainer Lukara wakata akizungumza kwenye uzinduzi wa
sherehe za wiki ya wazazi mkoani humo zilizofanyika kwenye kijiji cha
Malongwe na Swaila kwenye kata ya Mkwamba wilayani Nkasi mkoani humo.
Akisoma taarifa ya Mwenyekiti huyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
CCM Clement Bakuli alisema kuwa Rukwa ni moja ya mikoa michache nchini
ambayo ina fursa nyingi za uwekezaji katika nyanja mbalimbali zikiwemo
za kielimu ambazo hazijatumika ipasavyo na zinahitaji uwekezaji wenye
tija hivyo wananchi wanapaswa kuwakaribisha wawekezaji kwenye sekta
hiyo.
"Elimu ndio chachu ya mafanikio ya kila kitu hivyo sasa lazima
tukubali kukaribisha wawekezaji kwenye eneo hilo ili watusaidie kuwekeza
kwa kujenga, shule za msingi na za sekondari sambamba na vyuo vya kutoa
elimu ya juu vyenye kutoa elimu yenye kuleta tija kwa vijana
wetu......kupitia uwekezaji huo ndio tutapata wataalamu mbalimbali
wakiwemo wa idara ya afya, elimu na wengineo ambao kwa sasa tunawapata
kwa shida kutokana na wengi wao kukataa kufanya kazi katika mkoa wetu"
alisema
Aliongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa jitihada kadhaa za kuwashawishi
watumishi wa kada hizo, ikiwemo ya kuwepo kwa mfuko wa kumotisha
watumishi ili wakubali kwenda Rukwa kufanya kazi lakini wamekuwa
wakigoma hata wanaokubali kukaa kwa kipindi kifupi kisha ulazimika
kuondoka kwa madai ya mazingira magumu ya kazi.
"tusiwe na fikra potofu za kuogopa na kukataa uwekezaji kwani
hatutapata maendeleo yoyote ya kwetu binafsi wala ya mkoa..........
tuwakaribishe na tuingie nao ubia, naamini kwa kuwa wenzetu wanakuwa
wamejiandaa vizuri kiuchumi utaona kasi ya maendeleo itakavyokuwa kubwa
ukilinganisha na sasa hivi" alisema Lukara ambaye pia ni mfanyabiashara
maarufu mjini hapa.
Mkoa wa Rukwa ni moja ya mikoa katika ukanda wa ziwa Tanganyika
ambayo imetangaza vivutio vya uwekezaji katika nyanja mbalimbali ikiwemo
ya elimu ambapo hasa bado kasi ya uwekezaji kwenye elimu si ya
kuridhisha kwani mkoa huo una shule za msingi 357 na za sekondari 89
pekee kitu ambacho bado kinaonyesha kuhitaji wawekezaji kwenye eneo
hilo.
Awali, akisoma risala kwenye sherehe hizo mkazi wa kijiji hicho
Isack Lyande alisema kuwa shule ya msingi kwenye kijiji hicho
inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kukosa madarasa matatu
hivyo kusababisha wanafunzi wengine kusomea chini ya miti.
Alitaka serikali kuliangalia suala hilo na kuona namna ya
kulitafutia ufumbuzi wa kudumu kwani chachu ya kuathiri maendeleo ya
kitaaluma ya mwanafunzi na imekuwa ikiwakatisha tamaa na walimu kutoa
elimu yenye ubora.
Home »
» WADAU wa maendeleo mkoani Rukwa wametakiwa kuchangamkia fursa za uwekezaji hususani katika sekta ya Elimu
0 comments:
Post a Comment