Home » » RC:Marufuku kuingiza mifugo Katavi

RC:Marufuku kuingiza mifugo Katavi


Mussa Mwangoka, Katavi
 MKUU wa Mkoa wa Katavi, Dk Rajab Rutengwe amepiga marufuku uingizaji kiholela wa makundi ya mifugo mkoani humo ikiwa ni jitihada  zake kukabiliana na migogoro ya mara  kwa mara, baina ya wakulima na wafugaji.

Rutengwe alitoa kauli hiyo jana alipofungua mafunzo yaliyolenga kuwaondoa kwa hiari baadhi ya wananchi waliovamia hifadhi za misitu katika Tarafa ya Inyonga, Wilaya ya Mlele mkoani humo.

Alisema kuwa migogoro baina ya wakulima na wafugaji pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanyika hivi sasa maeneo hayo kwa kiasi kikubwa unachangiwa na uingizwaji holela wa makundi ya mifugo yanayoingia mkoani humo.

Alifafanua kuwa makundi hayo yanayoingizwa wialayani humo ni makubwa yakitokea mikoa ya jirani ya Tabora, Shinyanga na Mwanza.

"Ili kudhibiti uharibifu huo wa mazingira na migogoro ya wakulima na wafugaji, ni marufuku kwa madiwani, watendaji vijiji na vitongoji kutoa vibali vya ukataji wa misitu na uingizwaji wa mifugo mkoani Katavi," alisema.

Alisema utoaji wa vibali hivyo bila kufuata taratibu ulisababisha uvunaji wa kiholela wa misitu ambao umeanza kuleta athari mbaya kimazingira.

Mkuu huyo wa mkoa alibainisha kuwa walio na mamlaka ya kutoa vibali hivyo kwa sasa ni Kamati za Mazingira za Kata na Vijiji.

Aliongez kuwa hali hiyo itasaidia kuwapo kwa utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
  
"Nina  taarifa za uhakika kuwa upo ushahidi wa kutosha unaoonesha kuwa  wapo baadhi ya watendaji wa kata na vijiji wamekuwa wakituhumiwa wakichukua pesa kwa  wafugaji na hatimaye wanaruhusu makundi makubwa ya  ngÕombe  kuingia katika maeneo yao hivyo  kusababisha migogoro  ya wakulima  na wafugajiÕ Alisema.

Alidokeza kuwa atawasiliana na uongozi wa Mkoa wa Rukwa kuona namna ya kushirikiana kupambana na baadhi ya watu waliovamia na kuchoma moto misitu iliyopo kwenye Mlima wa Lyamba lya Mfipa uliopo mpakani mwa Mikoa ya Katavi na Rukwa.
Chanzo: Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Katavi yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa