Na Walter Mguluchuma.
Katavi
Mkoa wa Katavi umeendelea kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto kwa kuhakikisha kuwa afya ya mama inaimarika wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua mtoto .
Hayo yalisemwa hapo juzi na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dr Yahaya Hussein wakati akisoma taarifa ya Mkoa wa Katavi ya utekelezaji wa shughuli za Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia ,Wazee na Watoto kwa Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia , Wazee na Watoto Dr Faustine Ndungulile.
Kutokana na uboreshaji huo idadi ya wajawazito wanaojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya imeongezeka kutoka wajawazito 17,334 kwa mwaka 2012 sawa na asilimia 50 hadi 17,411 sawa na asilimia 79 kufikia septemba 2017 lengo la Mkoa ni kufikia asilimia 87 ifikapo Desemba 2018.
Alisema Mkoa wa Katavi umefanikiwa kutenga vyumba kwa ajiri ya huduma za damu salama tangu Desemba 2015 katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda ,Hospitali tarajiwa ya Halmashauri ya Mlele na kituo cha afya Karema .
Katika kipindi cha januari hadi Desemba 2017 jumla ya chupa 4,747 za damu zilikusanywa sawa na asilimia 87.9 lengo ilikuwa ni kukusanya chupa 5,399 kwa mwaka za damu kwa ajiri ya dharula za uzazi na wagonjwa wengine .
Dr Yahaya alieleza kuwa Mkoa umeendelea kutekeleza mpango wa kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambapo kwa kipindi cha januari hadi june 2017 wajawazito 28,603 walihudhuria kiliniki na kati yao 25,955 walipimwa maambukizi ya VVU wakati wa ujauzito sawa na asilimia 90.7 ya wajawazito wote waliohudhuria kiliniki.
Aidha jumla ya wajawazito 603 waligundulika kuwa na maambukizi sawa na asilimia 2.3 ambapo Mkoa umefanikiwa kutowa mafunzo ya namna ya kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa watowa huduma za afya 372 kutoka katika vituo 72 vya kutolea huduma za afya na pia wakunga 123 walipatiwa mafunzo ya huduma za dharula wakati wa kujifungua.
Naibu Waziri Dr Faustine Ndungulile alisema Serikali haitaki kusikia mtu anae kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya anakosa dawa kwani Serikali imeongeza bajeti ya dawa kwa Mkoa wa Katavi kutoka milioni 300 hadi kufikia zaidi ya shilingi bilioni mbili .
Alisema pia Serikali imeongeza bajeti ya dawa hapa nchini kutoka shilingi bilioni 30 hadi kufikia shilingi bilioni 270 ikiwa ni ongezeko la mara tisa ya bajeti ya awali .
Alizita Halmashauri kuweka utaratibu wa kulipa motisha wakunga wa jadi wkwani wamekuwa wakitowa msaada mkubwa sana katika kuokoa uhai wa mama na mtoto hivyo ni budi Halmashauri zikawawezesha kwa kuwanunulia vitendea kazi.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment