Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mpanda imekusanya zaidi ya sh. milioni
260 zilizotokana na mapato ya ndani zilizokusanywa na Idara ya
Ardhi na Maliasili katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Julai
2013 hadi Juni 2014.
Haya yalielezwa juzi na Kaimu Ofisa Ardhi na Maliasili na
Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Josephina
Rupia wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za idara hiyo
kwa kipindi cha mwaka 2013 na 2014 kwenye mkutano mkuu wa mwaka
wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda uliofanyika
kwenye ukumbi wa Maji mjini hapa.
Alisema Idara hiyo imeweza kukusanya jumla ya sh. 265,290,050 kwa
kipindi cha Julai 2013 hadi Juni mwaka huu zilizotokana na mapato
ya ndani.
Rupia alifafanua sh. 260,780, 000 zilitokana na ushuru wa
leseni za mbao, sh. 210,750 ushuru wa magobole, sh. 296,500 ushuru wa
asali na kuingia porini, sh. 914,000 ada ya fomu za viwanja na sh.
3,868,800 ushuru wa uwindaji wa kienyeji.
Alisema katika kipindi hicho cha mwaka mmoja idara hiyo
imeweza kufanya doria mbili kubwa na kufanikiwa kukamata mbao na
magogo yaliyovumwa bila kibali pamoja na magunia 369 ya mkaa na
wanazishikilia baiskeli tisa ambazo wavunaji haramu wa maliasili
walikimbia na kuziacha. Pia wamekamata ng’ombe 280 ambazo zilikuwa
zimeingizwa kwenye msitu wa hifadhi wa Nkaba na wamiliki watatu wa
mifugo hiyo wamefunguliwa mashitaka na kufikishwa mahakamani.
Josephina Rupia alilieleza baraza hilo na madiwani walikuwa
wakiongozwa na mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Yassin
Kibiriti idara hiyo imeweza kufanya operesheni ya kuondoa makazi
holela na watu 361 wameondolewa kwa nguvu na kati yao 15
wamefikishwa mahakamani.
Alifafanua idara hiyo imefanya mpango bora wa matumizi ya
ardhi katika Kijiji cha Lwega, Tarafa ya Mwese na wanatarajia
kuendelea katika vijiji vya Katuma na Kapanga.
Alisema wametatua baadhi ya migogoro ya mipaka kwenye baadhi ya
vijiji kwa kuzikutanisha pande zote mbili zilizokuwa na migogoro ya
kugombea mipaka kwenye vijiji vyao.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment