Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amepokea msaada wa pikipiki 44 kutoka Ubalozi wa China na Kampuni ya Fu-Tang ya nchini humo.
Msaada huo alikabidhiwa juzi mbele ya viongozi wa Wilaya ya Mlele
Mkoa wa Katavi katika hafla fupi iliyofanyika Kijiji cha Kibaoni.
Akizungumza na viongozi wa wilaya hiyo pamoja na wakazi wa kijiji
hicho kabla ya kukabidhi msaada huo, Balozi wa China nchini, Dk. Lu
Youqing, alisema anaamini kupatikana kwa pikipiki hizo kutasaidia kuleta
maendeleo ya haraka ya wilaya hiyo.
“Tunataraji matumizi ya pikipiki hizi yatasaidia kuleta maendeleo
ya haraka na hatimaye kuongeza kipato cha wakazi wa wilaya hii,” alisema
Balozi Lu ambaye ofisi yake imekabidhi pikipiki 20.
Alisema raia wa nchi yake wanafikia bilioni 1.3 na yeye anatamani
kuona walau kila mmoja akinunua walau kilo moja ya chakula kutoka
Tanzania ili waweze kuongeza soko kwa mazao yanayozalishwa na wakulima
wa Tanzania.
Naye Meneja Mkuu wa kiwanda cha kutengeneza pikipiki cha FEKON
ambayo ni kampuni tanzu ya Fu-Tang, Zheng Bing, alisema taratibu
zitakapokamilika, wana lengo la kujenga kiwanda cha kutengeneza pikipiki
na kompyuta ili kuongeza ajira kwa Watanzania. Kampuni hiyo ilikabidhi
pikipiki 24.
Akipokea msaada huo, Waziri Mkuu alimshukuru Balozi Lu na kampuni
ya Futang na kuahidi kuzigawa ili ziwasaidie watendaji kusimamia kazi
hivyo kuharakisha kuleta maendeleo kwa wakazi wa wilaya hiyo.
" Tuna kata 24 kwenye wilaya yetu kwa hiyo kila kata itapewa
pikipiki moja. Hiyo pikipiki siyo ya Katibu Kata binafsi bali ni ya
kata, kwa hiyo Katibu Kata atakuwa ndiyo msimamizi,” alisema Pinda
ambaye . yuko kijijini kwake Kibaoni kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
Alisema pikipiki saba zitapelekwa kwenye vituo vitano vya afya vya
Mamba, Usevya, Inyonga, Katumba na Kanoge na zahanati za Nsimbo na
Kasansa.
“Pia tutapeleka pikipiki nyingine nane katika shule za sekondari za
Sitalike, Machimboni, Magamba, Nsimbo na Mtapenda. Nyingine ni Utende,
Inyonga na Kasokola,” aliongeza.
Wengine watakaofadika na mgao huo ni watendaji wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wa Wilaya hiyo kwa kila mmoja kupatiwa moja, jumuiya za
chama tatu na moja iliyobakia itagawiwa kwa CCM Mkoa wa Katavi.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment