UMOJA wa Azaki umesema ipo haja ya kuendeleza na kudumisha Muungano na kuwepo na serikali tatu.
Wakitoa tamko la pamoja katika maazimio yaliyofikiwa wakati wa
kongamanano la siku tatu jijini Dar es Salaam jana, walisema wamefikia
uamuzi huo baada ya kuona Muungano ni moja ya maudhui ambayo yamekuwa
yakibishaniwa katika mchakato wa uundwaji wa Katiba mpya.
Akisoma maazimio kwa niaba ya Azaki hizo, Mjumbe wa Baraza la Wazee
Wastaafu Zanzibar, Baraka Shamte, alisema wamekubaliana mambo kadhaa
yawe ya Muungano ikiwemo katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Ulinzi na usalama, uraia na uhamiaji, sarafu na Benki Kuu.
Masuala mengine waliyokubaliana yawepo kwenye Muungano ni Mambo ya
Nje, usajili wa vyama vya siasa, ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya
kodi yatokanayo na mambo ya muungano, usimamizi wa ardhi, masuala ya
elimu ya juu na Mahakama ya Rufaa.
Kuhusu Bunge Maalumu, alisema Azaki inatoa wito kwa mamlaka ya nchi
kuhakikisha idadi ya uwakilishi wa wajumbe wa Bunge Maalumu
inawakilisha makundi yote ya jamii kwa usawa.
“Ili kuleta dhana ya usawa na ulinganifu wa Tanzania Bara na Tanzania
Visiwani, idadi ya wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba iwe nusu kwa
nusu kati ya Tanganyika na Zanzibar kama ilivyo kwenye Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
“Hii ni kwa sababu Tanzania ni muungano wa Tanganyika na Zanzibar
hivyo kupata Katiba mpya itakayoiongoza Tanzania mchakato lazima uwe
wa kidemokrasia na usawa kati ya nchi na washiriki kwani itasaidia
kupata maamuzi ya theluthi mbili ambayo yatakuwa na uwakilishi sawa
wakati wa kupiga kura kwenye Bunge Maalumu la Katiba,” alisema
Shamte.
Akizungumzia ushiriki wa wananchi na elimu ya Katiba kwa umma, Azaki
hizo zilisema muda wa kupeleka elimu kabla ya kupiga kura hautoshi,
hivyo unahitajika muda wa kutosha takriban miezi mitatu ya kutoa elimu
kuhusu kupiga kura, elimu kuhusu Bunge Maalumu la Katiba na elimu ya
uraia, ili kuwajengea wananchi uwezo na ufahamu katika suala zima
la mchakato wa Katiba.
Kongamano hilo lililozikutanisha Azaki 300 kutoka mikoa yote ya bara
na visiwani, limeandaliwa kwa ushirikiano wa Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Katiba, Mtandao wa Jinsia (TGNP) na
Baraza la NGOs.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment