Friday, November 29, 2013

Azaki zaunga mkono serikali tatu

UMOJA wa Azaki umesema ipo haja ya kuendeleza na kudumisha Muungano na kuwepo na serikali tatu.
Wakitoa tamko la pamoja katika maazimio yaliyofikiwa wakati wa kongamanano la siku tatu jijini Dar es Salaam jana, walisema wamefikia uamuzi huo baada ya kuona Muungano ni moja ya maudhui ambayo yamekuwa yakibishaniwa katika mchakato wa uundwaji wa Katiba mpya.
Akisoma maazimio kwa niaba ya Azaki hizo, Mjumbe wa Baraza la Wazee Wastaafu Zanzibar, Baraka Shamte, alisema wamekubaliana mambo kadhaa yawe ya Muungano ikiwemo katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na usalama, uraia na uhamiaji, sarafu na Benki Kuu.
Masuala  mengine waliyokubaliana yawepo kwenye Muungano ni  Mambo ya Nje, usajili wa vyama vya siasa, ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya muungano, usimamizi wa ardhi, masuala ya elimu ya juu na Mahakama ya Rufaa.
Kuhusu Bunge Maalumu, alisema Azaki inatoa wito kwa mamlaka ya nchi kuhakikisha idadi ya uwakilishi wa wajumbe wa Bunge Maalumu inawakilisha makundi yote ya jamii kwa usawa.
“Ili kuleta dhana ya usawa na ulinganifu wa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, idadi ya wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba iwe nusu kwa nusu  kati ya Tanganyika na Zanzibar kama ilivyo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Hii ni kwa sababu Tanzania ni muungano  wa Tanganyika na Zanzibar hivyo kupata Katiba mpya  itakayoiongoza Tanzania mchakato lazima uwe wa kidemokrasia na usawa kati ya nchi na washiriki kwani itasaidia kupata maamuzi ya theluthi mbili ambayo yatakuwa na uwakilishi sawa wakati wa kupiga kura  kwenye Bunge Maalumu la Katiba,” alisema Shamte.
Akizungumzia ushiriki wa wananchi na elimu ya Katiba kwa umma, Azaki hizo zilisema muda wa kupeleka elimu kabla ya kupiga kura hautoshi, hivyo unahitajika muda wa kutosha takriban miezi mitatu ya kutoa elimu kuhusu kupiga kura, elimu kuhusu Bunge Maalumu la Katiba na elimu ya uraia,  ili kuwajengea  wananchi  uwezo na ufahamu  katika suala zima la mchakato wa Katiba.
Kongamano hilo lililozikutanisha Azaki 300 kutoka mikoa yote ya bara na visiwani, limeandaliwa kwa  ushirikiano wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Katiba, Mtandao wa Jinsia (TGNP) na Baraza la NGOs.
Chanzo;Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment