Home » » KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AKATAA MIRADI MPANDA, NI ILE ILIYOJENGWA CHINI YA KIWANGO

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AKATAA MIRADI MPANDA, NI ILE ILIYOJENGWA CHINI YA KIWANGO

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Stella Manyanya akiwa na wakimbiza mwenge kitaifa wakikimbiza mwenge huo kuelekea upande wa pili waliopo viongozi wa Mkoa wa Katavi (hawapo pichani) tayari kwaajili ya kuukabidhi jana kwenye kijiji cha Stalike, Picha na Mussa Mwangoka
Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya akimkabidhi mwenge wa uhuru mkuu wa mkoa wa Katavi, Rajabu Rutengwe makabidhiano ambayo yalifanyika katika eneo la Stalike wilayani Mpanda jana baada ya mwenge huo kumaliza kukimbizwa mkoani Rukwa. Picha na Mussa Mwangoka
Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Honest Mwanossa akizungmza na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda (hawapo pichani) jana kuhusu udhaifu wao katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo hali inayosababisha kujengwa chini ya kiwango pembeni yake ni mkuu wa wilaya hiyo Paza Mwamlima. Picha na Mussa Mwangoka
 

Mussa Mwangoka, KataviYetu
UWAJIBIKAJI mdogo na kukithiri kwa rushwa miongoni mwa baadhi ya madiwani na watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda mkoani Katavi ni sababu tosha inayochangia miradi mingi ya maendeleo kutekelezwa chini ya kiwango.

Kiongozi wambio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, Honest Mwanossa alisema hayo jana mara baada ya kukagua na kukataa kuipokea baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo inapitiwa na mbio za mwenge wa uhuru mkoani humo.

Miradi ambayo aliikataa ni ile ya ujenzi wa ofisi ya Mbunge jimbo la Mpanda vijiji ambayo alidai imejengwa chini ya kiwango ambapo fedha iliyotumika haifanani na thamani ya jengo hilo.
Pia amekosoa ujenzi wa miradi kadhaa na kutaka kasoro zilizojitokeza ikiwamo kuwa na nyufa zinarekebishwa na wakandarasi waliotekeleza miradi hiyo haraka iwezekanavyo.

Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge, licha ya kukataa kupokea majemgo hayo pia alimtaka mkurugenzi wa wilaya hiyo kutoa maelez0 ya kina kwanini hali hiyo inajitokeza, huku mhandisi wa wilaya akikacha msafara huo ili kukwepa hoja zilizokuwa zikimkabili kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo.

Alisema kuwa tabia ya baadhi ya watendaji kuchukua asilimia kumi "ten percent" kutoka kwa wakandarasi waliopewa zabuni imekuwa sugu kwa sasa hali ambayo inachangia miradi mingi ya maendeleo kutekelezwa ikiwa chini ya kiwango na kutofanana na fedha halisi inayotajwa kutumika.

Katika hatua nyingine aliwataka madiwani kuacha udhaifu katika kusimamia vizuri rasilimali fedha ndani ya halmashauri zao kwani kutofanya hivyo kunatoa mwanya watendaji wasio waaminifu ambao sasa wamegeuka mchwa na kutafuna rasilimali hizo kwa kutokuwa wazalendo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mwanossa aliongeza kuwa watendaji wasio waaminifu kamwe hawatafumbiwa macho kwa kuwa ndio wanaoichafua Serikali mbele ya wananchi kwa kutekeleza miradi mibovu, hivyo wanapaswa kubadilika mara moja kabla hatua za kuwashughulikia hazijaanza kuchukuliwa kwani wameanza kufahamika.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa katavi, Dk Rajab Rutengwe,  akisoma taarifa ya mkoa  baada ya  kupokea mwenge  kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ,Mhandisi  Stella Manyanya  katika kijiji  cha Sitalike alisema  mwenge wa uhuru  ukiwa mkoani  humo  utapitia miradi 34 yenye thamani ya Sh 2,225,855,250- ambayo  itakaguliwa  kuwekewa mawae ya msingi , kuzinduliwa  na kufunguliwa.

Alisema wananchi  wamechangia Sh 398,547,241- huku Halmashauri  zikiwa  zimechangia  Sh 1,298,842,859-, wahisani  na wadau  wengine wa maendeleo  Sh 176,265,150- na Serikali  Kuu  Sh 352,200,000-.

Kwa mujibu wa Dk Rutengwe, baada ya  kuhitimisha   mbio  zake  katika  mkoa  wa Katavi , mwenge utakabidhiwa  kwa uongozi  wa  mkoa  wa Tabora  Septemba 22, mwaka  huu kijijini Ipole katika  wilaya  ya Sikonge.
Blogzamikoa

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Katavi yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa