Home » » UJASIRI WA WANAWAKE SILAHA YA KUTOKOMEZA VITENDO VYA KIKATILI DHIDI YAO NA WATOTO - RC.

UJASIRI WA WANAWAKE SILAHA YA KUTOKOMEZA VITENDO VYA KIKATILI DHIDI YAO NA WATOTO - RC.

Walter Mguluchuma.
Katavi

WANAWAKE mkoani Rukwa wametakiwa kuwa  jasiri na kuacha nidhamu ya woga kwa waume zao na badala yake wawe utamaduni wa kuripoti polisi kuhusu  vitendo vya unyanyasaji wa kikatili unaofanywa dhidi yao ili kusaidia harakati za kupiga vita vitendo hivyo katika jamii.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya alisema hayo jana wakati akizindua kituo kidogo cha polisi katika kijiji cha Tunko kilichopo wilayani Sumbawanga, kituo ambacho kimejengwa kwa msaada wa taasisi ya Mfuko wa Changamoto za MileniaTanzania (MCA-T) iliyofadhili pia ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga.

Manyanya alisema kuwa imefika wakati sasa wanawake wanapaswa kujitambua kuwa wao ndio silaha ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, hivyo wana wajibu wa kutumia fursa ya kusogezewa vituo vya polisi katika maeneo yao ili  kutoa taarifa ambazo zitakuwa chachu ya kukomesha vitendo hivyo katika jamii.

"Nendeni polisi mkaripoti kuhusu kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kikatili dhidi ya wanawake na watoto.......niwahakikishieni kwamba kule mtasikilizwa kupitia madawati ya jinsia na hatua zitachukuliwa sio kukaa kimya kwani kufanya hivyo mnaendelea kufumbia macho tabia hii ambayo tunaipinga katika jamii" alisema Manyanya

Alisisitiza kwamba kushamiri kwa vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake na watoto ambavyo mara kadhaa vimesababisha mauaji ni matokeo ya watendewa wengi wao kutokuwa na uelewa kujua wapi wanapaswa kupeleka malalamiko yao.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema kuwa ujenzi wa vituo hivyo viwili vya polisi ni chachu ya kutaongeza ari ya utendaji wa polisi hivyo kuwafanya afanye kazi zao ufanisi mkubwa wenye kuleta tija kwa jamii wanayoihudumia.

Mwaruanda aliongeza kuwa pamoja na kuwa na vituo hivyo vya kisasa lakini bado ushirikiano baina polisi na wananchi unahitajika hasa katika kutoa taarifa za siri kuhusu uhalifu kwani ndio utasaidia kudhibiti hali hiyo.

Awali, Naibu afisa wa mtendaji wa mkuu wa MCA-T, Paschal Assey alisema kuwa lengo la kujenga vituo hivyo vya polisi vilivyogharimu zaidi ya Sh milioni 379 ni kuimarisha usalama wa raia pamoja na mali zao katika maeneo yanayopitiwa na barabara ya Tunduma - Sumbawanga ambayo unatembea umbali mrefu bila kuwepo kwa kituo chochote cha polisi kitu ambacho si sahihi.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Katavi yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa