Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
- Ndugu wa wazazi watwangana, wafukia kaburi tupu
MTAFARUKU mkubwa umetokea msibani katika Mtaa wa Kawajense
Madukani, Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi baada ya ndugu wa pande mbili
kugombania kuuzika mwili wa kichanga, Junia Bacho mwenye mwaka mmoja na
nusu aliyefariki juzi, katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda.
Tukio hilo ambalo lilivuta hisia za watu wengi, lilitokea juzi katika
mtaa huo baada ya mtoto huyo kufariki akiwa amelazwa katika hospitali
ya wilaya ambako alikuwa akiuguzwa na shangazi yake, Evelyne Komba.
Baada ya mtoto huyo kufariki, kulitokea kutoelewana baina ya ndugu wa
baba wa mtoto, Joseph Bacho na ndugu wa mama aitwaye Anna Kizo.
Upande wa ndugu wa baba ulidai ndio wenye haki na jukumu la kuchukua
mwili wa marehemu na kuupeleka nyumbani kwa mama mzazi wa baba wa
marehemu aitwaye Ted Francis anayeishi katika Mtaa wa Madukani mjini
hapa.
Ndugu wa mama wa marehemu nao walidai hawako tayari kuona msiba huo
unakwenda kwa baba wa mtoto kwani hakuwa na uhalali wa kuuchukua kwa
kile walichodai kwamba alikuwa hajatoa mahari na hivyo wao hawamtambui.
Hali hiyo iliwafanya ndugu wa pande hizo mbili kuanza kutupiana
shutuma ambapo wale wa baba mtoto walidai mama yake alishindwa
kumuhudumia wakati akiwa mgonjwa, na kwamba muda wote baba alipokuwa
akifika nyumbani, alikuwa hamrusu kumwona mwanae.
Kwamba mtoto huyo alipochukuliwa na baba yake Juni 18 kwa ajili ya
kushughulikia matibabu ya ugonjwa wake wa ukosefu wa lishe (kwashakoo),
mama hakuwahi kufika kumwangalia, hali iliyolazimu aangaliwe na
shangazi na bibi yake.
Pamoja na maelezo hayo, ndugu wa upende wa mama wa marehemu
waliendelea na msimamo wao wa msiba kuwa kwao, ingawa baada ya
mabishano ya muda mrefu pande hizo ziliamua kuuacha mwili hospitali.
Baada ya kurudi nyumbani kila upande uliweka msiba, hali iliyofanya kuwepo na misiba sehemu mbili katika mtaa mmoja.
Siku iliyofuata, wazee wa mtaa waliingilia kati kwa kufanya kikao na
pande hizo zilizokuwa zikivutana, kisha kufikia uamuzi wa kupeleka
msiba huo nyumbani kwa baba wa marehemu.
Kufutia uamuzi huo, shangazi wa marehemu, Evelyne aliongoza ndugu
kwenda kuuchukua mwili wa marehemu tayari kwa ajili ya mazishi
yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kwenye makaburi ya Kawanjense Msufini.
Hata hivyo, wakati shughuli za mazishi zikitarajia kuanza, ndugu wa
baba wa marehemu walipata taarifa kuwa kaburi walilochimba kwa ajili ya
kuzikia mwili wa mtoto huyo limefukiwa.
Ndugu hao, walipofika makaburini walikuta mama mkubwa wa marehemu
aitwaye Jane Kiza na wenzake wakiwa wanamalizia kulifukia kaburi hilo.
Jane na kundi lake walipoulizwa kwanini wamefukia kaburi hilo,
walianza kufoka na kisha kundi la ndugu wa mama wa marehemu walitokea na
kuanza kuwashambulia kwa kipigo ndugu wa baba.
Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiongozwa na SSG Bahati
walifika eneo hilo na kutuliza ghasia kisha walielekea msibani na
kuamuru mwili huo urudishwe kuhifadhiwa hospitali hadi hapo ufumbuzi
utakapokuwa umepatikana.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment