BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Nsimbo, Wilaya ya Mlele,
Katavi, limepiga marufuku ugawaji wa mbegu zinazotolewa kwa vocha za
ruzuku aina ya PANA 4 M 19 katika halmashauri hiyo kutokana na mbegu
hizo kutokuwa na ubora.
Uamuzi huo ulitolewa hapo juzi kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Nsimbo.
Madiwani wa halmashauri hiyo walitoa malalamiko ya mbegu hizo
kutokuwa na ubora na kufanya zishindwe kuota na kuwasababishia wakulima
hasara.
Diwani wa kwanza kutoa malalamiko alikuwa ni Diwani wa Kapalala,
Rewards Sichone, aliyeeleza kwamba wakulima wa kata yake walichukua
mbegu za mahindi aina ya Pana zinazotengezwa mkoani Arusha ambazo
zimeshindwa kuota kutokana na kukosa ubora.
Alieleza pia mawakala wa pembejeo wamekuwa wakiwauzia wakulima
pembejeo bila kubandika bei kwenye maduka yao na matokeo yake wamekuwa
wakiuza bei kubwa kuliko iliyopangwa na serikali.
Sichone alitoa mfano wa bei ya mbolea aina ya UREA ambayo wakala
badala ya kuuza kwa sh 20,500 yeye anauza sh 26,500 na kwamba baada ya
kugundua alimfuata wakala huyo na kumtaka awarudishie kiwango cha fedha
alichowazidishia. Tayari wakala huyo ameanza kurudisha fedha hizo kwa
wakulima.
Diwani wa Magamba, Philip Kalyalya, alieleza tatizo la mbegu kutoota
lipo pia kwenye kata yake, hivyo aliomba wakulima waliopanda mbegu
hizo na kushindwa kuota walipwe fidia na wakala anyang’anywe vocha zote
za ruzuku ili asilipwe fedha na serikali.
Diwani wa Kasokola, Crisanti Mwanawima alishauri kabla ya mbegu
kusambazwa kwa wakulima ziwe zinakaguliwa na wataalamu wa kilimo ili
kukabiliana na tatizo kama hilo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nsimbo, Mohamed Assenga, alitaka Ofisa
Kilimo wa halmashauri hiyo, Rodrick Ntulo, kueleza baraza hilo sababu
za mbegu hizo kushindwa kuota.
Ntulo alikiri kupokea kwa taarifa za mbegu hizo kutoka kata
mbalimbali na ndipo idara hiyo ya kilimo kupitia wataalamu wake
walipoamua kuzifanyia majaribio na kubaini hazikuweza kuota.
Alisema kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mlele ameishaanza
kuchukua hatua kwa kuwaandikia barua wakala mkuu wa pembejeo akimtaka
asisambaze na kugawa mbegu hizo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment