Tuesday, November 20, 2012

WIZARA YA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA KUONGEZA UWEZO WA MAGHALA YA KUHIFADHI AKIBA YA CHAKULA KUTOKA TANI 220,000 HADI TANI 400,000 KUFIKIA 2014‏


Na Walter Mguluchuma
Mpanda

SERIKALI  kupitia wizara ya kilimo, chakula na ushirika  imeweka mikakati ya kuhakikisha  wakala wa hifadhi ya chakula YA TAIFA (NFRA) inafikia uwezo wa kuhifadhi tani 400,000 za mahindi  kutoka tani 220,200 za sasa ifikapo mwaka 2014

Meneja wa NFRA  mkoa wa Rukwa , Amos  Mtafya   alisema hayo jana wakati wa hafla fupi  ya kuitimisha  rasmi zoezi  la uhamishaji  wa mahindi tani  20,000 za mahindi  lillilofanywa  na   askari wa Jeshi la Wananchi  wa Tanzania (JWTZ) ambapo Sherehe iliyofanyika  katika  Kituo  cha  NFRA mjini  Mpanda  mkoani Katavi

Askari  hao  wa JWTZ  kwa kutumia magari yao walihamisha tani  hizo za mahindi  kutoka  maghala ya kituo  cha  Sumbawanga mjini  na kuyapeleka  mjini Mpanda  mkoani Katavi ambapo  zoezi  hilo lilichukua  siku 87.

Kwa mujibu wa Mtafya  katika kutekeleza  wa suala hilo , Serikali  ya Tanzania  kwa kushirikiana na  Serikali ya  China wameingia mkataba  na Kampuni  ya Kichina  ya Jiam Gsu Muyang  Gropu Co. Ltd ambayo tayari  imeanza  kufanya  upembuzi yakinifu  kwa ajili  ya mradi huo.

Aliongeza kuwa  Kampuni hiyo  itajenga  silo  katika Kanda mbalimbali  nchini  zitazokuwa  na uwezo  wa kuhifadhi  tani 160,000 kwa wakati mmoja  ambapo  kwa  Kanda ya Sumbawanga mkoani Rukwa  imepangiwa  kujengewa  silo  zenye uwezo  wa kuhifadhi  tani  20,000 za mahindi  ambazo  zitajengwa  mijini Mpanda mkoani Katavi.

Akifafanua alisema kuwa takwimu zinaonesha  miaka mitatu  iliyopita kituo  cha Mpanda  mkoani Katavi, kimepokea  chakula cha hifadhi  ya tani 80,000 za mahindi  kwa ajili ya kusafirishwa  kwa njia ya reli  ya kati wakati  uwezo  wa sasa  wa kuhifadhi ni tani 5,000 tu ambapo  ujenzi  huo  ukapokamilika  utaweza  kwa wakati  mmoja kuhifadhi  tani  25,000 za mahindi .

Kwa upande wake Kanali  wa JWTZ, Remark Kiwovele  akimwakilisha Mkuu Majeshi nchini Jenerali Devis Mwamnyange  alisema kuwa  zoezi  hilo  limesimamiwa  na kuratibiwa  vizuri  na JWTZ  ambao  nao  kwa  upande wao  wamejifunza kuishi   kwa ushirikiano  na  Mamlaka  za uraiani

Lengo  la  kuhamisha akiba hiyo  ya chakula  ni  kurahisisha  usafirishaji wake  kwa njia ya reli  kwenda  mikoa ya  Kanda  ya kati na Ziwa  ikiwemo Tabora , Dodoma,Shinyanga,Simiyu, Mwanza , Kagera na Mara  ambayo mara nyingi  hukumbwa  na uhaba wa chakula.

No comments:

Post a Comment