MKURUGENZI wa Shirika la Umoja wa Watu wa Afrika (APAPO), Kapeele Mpundililwa (36) amehuku
miwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Katavi kwenda jela miaka
mitatu baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kujipatia kwa njia ya
udanganyifu zaidi ya Sh milioni 3.9 .
Mkurugenzi huyo ambaye ni mkazi wa mjini Namanyere wilayani Nkasi
katika mkoa wa Rukwa alipatikana na hatia hiyo baada ya kuwatapeli watu
144 kuwa angewaajiri katika shirika hilo.
Hakimu wa mahakama hiyo Odira Amworo alitoa hukumu hiyo jana mjini
hapa akisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka
pasipo kutia shaka yoyote kwamba mshitakiwa alitenda uhalifu huo.
Hakimu Amwolo alieleza kuwa miongoni mwa ushahidi uliomtia hatiani
mshitakiwa ni hati za waliotapeliwa ajira alizolipia kwenye benki,
akaunti iliyokuwa ikimilikiwa na mshitakiwa mwenyewe ambazo
ziliwasilishwa mahakamani kama kielelezo huku zikiwa na majina ya wote
waliotapeliwa.
Awali, Mwendesha Mashtaka, Mwanasheria wa Serikali Peter Maiko alidai
kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 23, mwaka huu kwa nyakati tofauti
wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo alifika wilayani Mpanda
na kujitambulisha kuwa ni Mkurugenzi wa APAPO ambapo alianza kutangaza
nafasi mbalimbali za ajira kwamba watakaofuzu wataajiriwa na shirika
hilo.
Ilielezwa kuwa miongoni mwa njia alizozitumia kujipatia kiasi cha
fedha hizo kwa udanganyifu aliwaagiza kila muombaji anayetaka kuajiriwa
na shirika hilo lazima kwanza alipe ada.
Mwanasheria wa Serikali Maiko alidai mahakamani hapo kuwa kwa ngazi
ya Mtaa na Wilaya muombaji alilazimika kulipa ada ya Sh 17,000 ili aweze
kusailiwa huku sifa ikiwa lazima awe amehitimu elimu ya msingi hadi
kidato cha nne huku katika ngazi ya mkoa ada ilikuwa Sh 160,000 na
muombaji awe na stashahada.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo alifanikiwa kuwatapeli
watu 144 ambao wote walilipa jumla ya Sh milioni 3.9 ikiwa ni ada ili
waweze kusailiwa na kuajiriwa na shirika hilo.
Kwa mujibu wa Mwanasheria wa Serikali, Maiko, fedha zote hizo
ziliingizwa kwenye benki, akaunti ambayo namba zake walipatiwa waombaji
na watu wanne waliokuwa wakimsaidia kazi mshtakiwa huyo. Ilielezwa kuwa
baada ya mshtakiwa huyo kukamatwa wasaidizi wake wanne walitorokea.
CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment