Na Walter Mguluchuma .
Katavi .
Wizara ya Maliasili na Utalii imewataka Wahifadhi wote kushirikiana na Mamlaka za Mikoa na Wilaya ili kuweza kukabiliana na tatizo la uvamizi wa maeneo ya hifadhi yanayofanywa kwa ajiri ya shughuli za kibinadamu hususani uvamizi wa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi .
Wito huo ulitolewa hapo jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Generali Gaudence Milanzi wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya uongozi kwa maafisa Wanyama pori yenye lengo la kuwafanya wafanye kazi kutoka mfumo wa kiraia na kuwa mfumo wa kijeshi yaliofanyika katika kituo cha mafunzo Mlele Mkoani Katavi .
Mafunzo hayo ya wiki sita yaliwashirikisha wahitimu 97 wakiwemo Maafisa wandamizi 20 na maafisa wa kati 77 wa kutoka Mamlaka ya Wanyama pori Tanzania TAWA..
Meja Gernerali Milanzi alisema hivi sasa uhifadhi unakabiliwa na tatizo la uvamizi wa maeneo ya hifadhi yanayofanywa kwa shughuli za kibinadamu hususani uvamizi wa mifugo kwenye maeneo ya ya hifadhi hivyo Wizara inatowa wito kwa Wahifadhi wote kushirikiana na Mamlaka za Mikoa na Wilaya husika kumaliza tatizo hilo.
Aliwaagiza wahitimu wa mafunzo hayo washirikiane na wakuu wao kupanga mipango itakayo washirikisha wananchi katika kumaliza tatizo la uvamizi wa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi na migogoro ya mipaka kati ya maeneo ya hifadhi na Vijiji.
Milanzi aliwaomba wananchi wote kuendelea kuheshimu sheria za nchi na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya hifadhi kwani kufanya hivyo watambue kuwa ni makosa .
Alisema kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni Wizara ya Maliasili na Utalii imeshuhudia baadhi ya matukio ya mmomonyoko mkubwa wa maadili hasa kwa watumishi wa kada ya Askari wao wenyewe kujihusisha na vitendo vya ujangili na mengine mambo yasiyo faa katika utumishi wa umma .
Alieleza kuwa mafunzo waliopatiwa wahitimu hao anaamini kuwa kwa kuwa wao ndio viongozi wakuu wa askari watakwenda kusaidia kurudisha nidhamu kwa askari na watumishi wa chini yao kwa kuwaelekeza mambo mazuri ya kujenga wanayotakiwa kuyafanya ili kuhakikisha kunakuwepo na uhifadhi endelevu wa maliasili za nchi .
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyama pori Tanzania Martin Loibooki alisema ulinzi wa rasilimali za Wanyama pori umeendelea kuimarika ndani na nje ya mapori ya akiba na tengefu sambamba na kuimarisha ukaguzi wa nyara katika maeneo ya mipakani kwa kushirikiana na wadau wengine.
Chini ya uongozi wa Wizara TAWA imeshirikiana na idara ya Wanyama pori ,TANAPA na mamlaka ya hifadhi Ngorongoro NCCA katika kutekeleza kazi mbalimbali .
Alizitaja baadhi ya kazi hizo kuwa ni kuandaa rasimu ya kanuni za jeshi usu katika sekta za wanyama na mistu na na kufanya mapitio ya sheria ya uhifadhi wanyama pori Namba 5 ya mwaka 2009.
Mwakilishi w Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Mgana Msindai alisema TANAPA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha rasilimali za nchi yetu zinalindwa kwa faida ya sasa na kwa vizazi vijavyo.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment