Waziri Mkuu Mizengo Pinda amezitaka ngazi mbalimbali za uteuzi
wa wagombea wa CCM kuwapa wananchi nafasi kuchagua watu wanaowataka ili
kuepuka kupoteza viti katika uchaguzi.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati
akiwahutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye Uwanja wa Mikutano wa Kashaulili, Mpanda mkoani hapa.
Pia alitumia mkutano huo kuaga jimboni humo
akisema muda wa kuendelea kuwa Mbunge wa Katavi umetosha na sasa
anatafuta kitu kingine cha kufanya.
Kwa mara ya kwanza, Pinda alichaguliwa kuwa Mbunge
wa Mpanda Mashariki (sasa Katavi) mwaka 2000 na ameongoza jimbo hilo
kwa mihula mitatu.
Kuhusu uteuzi
Akizungumzia uteuzi wa wagombea mbalimbali, Pinda
aliwaasa viongozi wa CCM kuwateua watu wanaofaa kugombea uongozi kwenye
nafasi mbalimbali wale ambao wanakubalika na wananchi na wawape nafasi
wananchi kuchagua mtu wanayemtaka.
Alisema haifai CCM kuwalazimisha kwa kuwachagulia
wananchi kiongozi wasiyemtaka... “Kumekuwa na tabia ya kuteua watu ambao
hawakubaliki kwa wananchi na matokeo yake watu hao wamekuwa wakishindwa
kwenye uchaguzi... acheni chuki, msiteue watu kuwania uongozi kwa ajili
ya kupewa pesa na urafiki,” alisema.
Pinda aliyetangaza ni ya kuwania urais kimyakimya,
aliwataka Watanzania kutowachagua watu wanaotaka kiti hicho na vile vya
ubunge na udiwani kwa kutanguliza fedha.
“Watu hao wanaotafuta uongozi kwa kutoa rushwa kwa
wananchi ni hatari, kuweni makini kwa kuchagua viongozi waadilifu
watakaoongoza kwa kutanguliza mbele utaifa kuliko masilahi yao binafsi.
“Wako watu wanaotaka uongozi kwa kuhonga
wapigakura, watu wa namna hiyo hawafai kuwa wagombea wa urais, ubunge na
udiwani kwa kuwa si waadilifu na wakishapata uongozi kamwe hawezi
kuwajali wananchi kwanza watataka kurudisha fedha walizotoa.
“Hakikisheni mnachagua viongozi ambao wanaweza
kuwaongoza kwenye maeneo yenu na siyo vinginevyo, achaneni na watu
wanaowapa pesa hao hawatawapeleka kokote badala yake watakuwa viongozi
wabinafsi kwa kutanguliza masilahi yao mbele na kuwasahau wananchi
waliowaweka madarakani,” alisema Pinda.
Alisema: “Watu wanaotaka uongozi kwa fedha,
wanapowaletea hizo pesa kuleni lakini mhakikishe wakati wa uchaguzi
hamwapigii kura.”
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment