Monday, July 14, 2014

MALIASILI WAKUSANYA ZAIDI YA MIL.260/- MPANDA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
HALMASHAURI ya  Wilaya  ya Mpanda  imekusanya zaidi ya sh. milioni 260  zilizotokana  na mapato ya  ndani  zilizokusanywa  na Idara  ya Ardhi  na Maliasili  katika kipindi  cha mwaka mmoja  kuanzia  Julai  2013  hadi Juni 2014.
Haya yalielezwa  juzi  na Kaimu  Ofisa   Ardhi na  Maliasili  na  Mazingira    wa Halmashauri ya Wilaya  ya Mpanda,  Josephina Rupia wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa  shughuli  za idara hiyo kwa kipindi  cha mwaka  2013 na 2014 kwenye  mkutano  mkuu wa  mwaka  wa Baraza  la Madiwani  wa Halmashauri ya  Wilaya ya Mpanda uliofanyika kwenye ukumbi wa Maji  mjini  hapa.
Alisema Idara hiyo  imeweza kukusanya jumla ya  sh.  265,290,050 kwa kipindi cha Julai 2013  hadi Juni mwaka huu zilizotokana  na  mapato ya  ndani.
Rupia alifafanua  sh.  260,780, 000 zilitokana  na  ushuru  wa leseni za mbao, sh.  210,750 ushuru wa magobole, sh.  296,500 ushuru wa asali na kuingia porini, sh. 914,000 ada ya fomu za viwanja  na sh.  3,868,800 ushuru wa  uwindaji wa kienyeji.
Alisema  katika  kipindi  hicho  cha mwaka mmoja  idara hiyo  imeweza kufanya  doria mbili kubwa  na kufanikiwa  kukamata  mbao  na magogo yaliyovumwa bila kibali  pamoja na magunia  369 ya mkaa na wanazishikilia baiskeli  tisa  ambazo wavunaji haramu wa maliasili walikimbia na kuziacha. Pia wamekamata ng’ombe  280  ambazo   zilikuwa zimeingizwa kwenye msitu wa hifadhi  wa  Nkaba  na wamiliki watatu  wa mifugo hiyo  wamefunguliwa mashitaka na kufikishwa mahakamani.
Josephina  Rupia alilieleza  baraza hilo na madiwani walikuwa wakiongozwa na mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Yassin Kibiriti  idara hiyo imeweza  kufanya operesheni  ya  kuondoa  makazi holela  na watu 361 wameondolewa kwa nguvu  na kati yao 15  wamefikishwa mahakamani.
Alifafanua  idara hiyo   imefanya  mpango  bora wa matumizi ya ardhi  katika  Kijiji  cha  Lwega,  Tarafa ya Mwese  na wanatarajia  kuendelea katika  vijiji  vya Katuma na  Kapanga.
Alisema  wametatua baadhi ya migogoro ya mipaka kwenye baadhi ya vijiji kwa kuzikutanisha  pande zote mbili  zilizokuwa  na migogoro ya kugombea mipaka kwenye vijiji  vyao.
Chanzo:Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment