WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ametembelea mradi wa umwagiliaji wa Ugalla na kusifu juhudi za wananchi wa kata hiyo katika wilaya mpya ya Mlele mkoani Katavi.
Alikuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ugalla kata ya Ugalla mara baada ya kukagua mradi huo akiwa katika siku ya nne ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi jana mchana.
Alisema anawashukuru wakazi hao kwa kuibua mradi huo ili waweze kunufaika na maji ya mto Ugalla ambao unapita jirani. Pia aliwataka waheshimu uamuzi wao wa kutoa eneo hilo kwa mradi ili kuepuka migogoro ya umilikaji wa kifamilia na kiukoo.
“Ninawasihi muelewane ili kuepuka migogoro ya maeneo. Mkishaanza kuvuna wako watakaodai kuwa hapa nilipewa na babu yangu, hapa nilipewa na babu wa babu, wataanza kudai fidia. Ni vema mkaelewana mapena juu ya umiliki wa enepo la mradi,” alisema.
Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo hilo, Mhandisi Mkazi wa Umwagiliaji Kanda ya Mbeya, Bw. Elibariki Mwendo alisema wamejenga tanki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 530,000 ambazo zinaweza kumwagilia hekta 225.
Alisema mitambo ya kupandisha maji kwenye tanki hilo itaendeshwa kwa kutumia nguvu ya umeme wa jua pamoja na umeme unaozalishwa kwa nguvu ya upepo.
Mradi huo ulioibuliwa na wananchi mwaka 2007 kupitia zoezi la fursa na vikwazo vya maendeleo, umegharimu sh. milioni 778. Unamilikiwa na wanachama 146 na utahudumia watu 3,077.
(Jumanne, Desemba 18, 2012) Waziri Mkuu atakwenda kata ya Sitalike ambako atahutubia wananchi.
0 comments:
Post a Comment