Na Walter Mguluchuma .
Katavi
Baadhi ya Wananchi wa Tarafa za Mwese Karema wakiwa na Madiwani wao wanapinga uamuzi uliotplewa na Uongozi wa Serikali wa Mkoa wa Katavi wa kuhamisha ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda kwa sasa Tanganyika kutoka Kata ya Katuma na kuhamishia Kata ya Tongwe.
Wananchi hao wamedai kuwa kitendo cha kuwahamishia ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri yao kutoka Kata ya Katuma na kuhamishia Kata ya Tongwe yanapingana na uamuzi wa kikao cha mashauriano cha Mkoa wa Katavi RCC kilichoamua ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri hiyo kuwa ni Kata ya Katuma ,
Diwani wa Kata ya Mwese Juma Hawazi akizungumza kwa niaba ya wananchi wake mbele ya wandishi wa habari hapo jana alisema wananchi wa Kata hiyo hawajaridhishwa wala kufurahishwa na uamuzi uliotolewa na uongozi wa Serikali wa Mkoa wa Katavi wa kuhamishia ujenzi wa Halmashauri hiyo Katika Kata ya Tongwe.
Alisema lengo la Serikali ni kusogeza huduma karibu na wananchi lakini eneo ambalo limependekezwa na Uongozi wa Serikali kuwa makao makuu ya Halmashauri lipo pembezoni na lipo jirani sana na Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda na Nsimbo .
Alieleza iliwekwa tume maalumu ya watalamu iliyokuwa ikifuatilia ni eneo lipi linalofaa ambapo kata ya Katuma ilipata alama nyingi na hivyo ilipitishwa na pia kikao cha mwisho cha RCC kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa mstaafu Dr Ibrahimu Msengi kilipisha makao makuu kuwa yawe Kata ya Katuma .
Mwenyekiti wa Kijiji cha Katuma Yassin Kapaya alisema wananchi wanajiuliza na kushangazwa na taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Genelali Mstaafu Raphael Muhuga kuwa makao makuu yatakuwa kata ya Tongwe kata ambayo ipo pembezoni .
Alisema wanajiuliza kama Rais alisha sema lengo la serikali yake ni kuwasogezea huduma wananchi ni vipi wananchi wa Halmashauri hiyo waendelee kuwa mbali na huduma .
Alifafanua kuwa wanashangazwa na sababu zinazotolewa na uongozi wa Serikali wa Mkoa wa Katavi kuwa eneo la Kata ya Katuma lipo karibu na vyanzo vya mto Katuma kitu ambacho sio sahihi kwani ukweli ni kwamba vyanzo vya mto vipo umbali wa kilometa 30 toka eneo ambalo lilipendekezwa kujengwa makao hayo ya Halmashauri .
Nae kiongozi wa mila wa kabila la Wabende Mtemi Mlela Malack alisema ameshangazwa na taarifa ya mabadiliko hayo ambayo ameyaona kuwa ni mapya na yasiyojali kumsogezea huduma mwananchi karibu
Alisema anashindwa kuelewa vigezo vilivyotumika kuhamisha ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri kutoka Katuma na kuwa Tongwe wakati Katuma ndio katikati na kuna njia za kuingia na kutoka .
Mtemi Malack alieleza kama lengo ni kusogeza huduma kwa wananchi yaani kila mwananchi aifuate huduma leo hii kwanini Kata ya Katuma iliyokatikati ya kata zote isiwe makao makuu ya Wilaya hiyo mpya ya Tanganyika .
Kwa upande wake Hamisi Kiboko alisema kuwa kitendo cha kuhamishia makao makuu Tongwe kutaifanya Manispaa ya Mpanda kuendelea kubeba mzigo wa kuwahudumia wagonjwa kwani hakuna mgonjwa atakae kuwa anatoka Karema mwese na Kabungu ambae atakuwa anakwenda Tongwe kutafuta huduma ya afya kulingana na jiografia ilivyo .
Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Generali mstaafu Raphael Muhaga alitangaza kuwa makao makuu ya Halmashauri hiyo yatajengwa Kata ya Tongwe na kwenye ziara ya Waziri Mkuu inayoanza kesho Mkoani Katavi amepangiwa kutembelea eneo hilo .
No comments:
Post a Comment