Na Walter Mguluchuma
Katavi
MWENYEKITI wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Mlele mkoani
Katavi Said Njiku ameliagiza jeshi la polisi wilayani humo kuwakamata na
kuwafikisha mahakamani baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kasansa ambao
wanatuhumiwa kuwazuia askari polisi kutekeleza majukumu yao.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa agizo hilo jana baada ya askari polisi wa
kituo cha Majimoto wilayani humo kushambuliwa kwa mawe na wananchi
wakati wakienda kumkamata mganga mmoja wa jadi maarufu kwa jina la
kamchape ambae wananchi hao walikuwa wamemwita kijijini hapo ili
awaondoe uchawi watu waliokuwa wakidaiwa kuwa ni wachawi.
Siku ya Mei 13 majira ya saa 8 za mchana polisi walipata taarifa za
siri kutoka kwa mmoja wa wakazi hao walifika katika kijiji hicho ili
kumkamata kamchape huyo ambaye alikuwa anafanya kazi ya kuwanywesha dawa
watu waliokuwa wakituhumiwa kuwa ni wachawi ili waache kuroga.
Akiwa anaendelea na kazi hiyo ghafla gari la polisi lilifika kijijini
hapo hali iliyowaudhi wananchi wakijua kuwa polisi wamefika kuzuia zoezi
hilo ndipo walipochukua mawe na kuanza kuwarushia polisi hao ambao
walikuwa wameongozana na mwananchi aliyewapa taarifa hali iliyosababisha
polisi hao kuzidiwa nguvu na kukimbilia katika ofisi ya kata.
Wananchi hao wakiwa wamejaa jazba walifika katika ofisi hizo na kupasua
vioo kwa mawe na kisha kuvunja mlango kitendo kilicho sababisha polisi
wakimbie na kisha kumpiga mwananchi aliyekwenda kutoa taarifa polisi na
kumjeruhi vibaya ambapo amelazwa hospitalini anapatiwa matibabu.
Kutokana na tukuio hilo ndipo mwenyekiti huyo wa ulinzi na usalama
alipofika kijijini hapo na kuitisha mkutano wa hadhara na kukemea
kitendo hicho na kuwaagiza polisi kuhakikisha wanawasaka watu wote
waliohusika na vurugu hizo ili sheria ichukue mkondo wake.
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho ambao wengi wao ni wanaume wamekimbia
nyumba zao pamoja na huyo kamchape ambapo wanaishi porini wakihofia
kukamatwa na polisi kutokana na maagizo aliyotoa mkuu huyo wa wilaya.
No comments:
Post a Comment