Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, amekataa ombi la wakazi wa jimbo lake la uchaguzi
la Katavi la kumtaka agombee tena ubunge katika jimbo hilo ili
kuendeleza mipango ya maendeleo aliyoianzisha.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari ilimnukuu Pinda
akijibu maombi ya wakazi hao baada ya Ibada ya Jumapili iliyofanyika
katika Kigango cha Kanisa Katoliki cha Kibaoni Wilaya ya Mlele mkoani
Katavi.
Pinda alisema anamshukuru Mungu kwa nafasi aliyopewa ya kulitumikia
Taifa akiwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na anaamini wakati umefika wa
yeye kuwaachia wengine nafasi ya ubunge wa Jimbo la Katavi.
Alisema ataendelea kuwa karibu na wakazi wa jimbo hilo wakati wote
na kwa vile atakuwa na muda wa kutosha kushiriki kikamilifu katika
mikakati ya kuwaletea maendeleo ili wajikwamue kutoka kwenye umaskini.
Kwa upande mwingine, Pinda aliwaasa wakazi wa jimbo hilo wawe
makini kuchagua mbunge na madiwani na kamwe watoa rushwa na wabadhirifu
wasipewe nafasi katika uchaguzi ujao utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Akimshukuru Waziri Mkuu, Paroko wa Parokia ya Usevya wilayani humo,
Padri Aloyce Nchimbi, aliwaasa wakazi wa Mlele kumuenzi Pinda hata
atakapokuwa amestaafu kwani bado watahitaji busara na uzoefu wake katika
kujiletea maendeleo.
Pinda yuko kijijini kwake Kibaoni ajili ya mapumziko mafupi na
alitoa msimamo wake huo jana ikiwa ni siku ya mwisho kwa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kutoa na kupokea fomu kwa makada wake wanaoomba
wateuliwe kugombea ubunge na udiwani katika uchaguzi huo
utakaovishirikisha pia vyama vya upinzani.
Msimamo huo wa Pinda umekuja siku chache baada ya jina lake kukatwa
katika kinyang'anyiro cha urais ndani ya CCM hivi karibuni mjini
Dodoma.
Pinda alikuwa kati ya wanachama 38 wa CCM waliojitosa katika kinyang'anyiro cha urais kwa tiketi ya chama hicho.
Hata hivyo, jina lake lilikuwa miongoni mwa majina yaliyokatwa kwa
mara ya kwanza na kubakia matano ambayo yalipelekwa kwenye Kamati Kuu
(CC) ya CCM.
Majina yaliyopelekwa kwenye kamati hiyo yalikuwa ni ya Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa
Ujenzi, Dk. John Magufuli, Dk. Asha-Rose Migiro, Balozi Amina Said Salum
na January Makamba.
Majina hayo yalipelekwa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM ambapo wajumbe wake walipitisha majina matatu kati ya matano.
Waliopenya katika kinyang'anyito hicho ni Dk. Magufuli, Dk. Migiro
na Amina na kupelekwa mbele ya Mkutano Mkuu na wajumbe kupiga kura na
kumpata Dk. Magufuli atakayepeperusha bendera ya chama hicho kumtafuta
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pinda aliteuliwa kushika wadhifa wa Uwaziri Mkuu na Rais Jakaya
Kikwete, baada ya aliyekuwa akishikilia wadhifa huo, Edward Lowassa,
kujiuzulu baada ya kuhusishwa na kashfa ya Richmond mwaka 2007.
SOURCE:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment