Friday, April 24, 2015

WANAENDELEA KUKAMATWA: AKAMATWA NA NYARA ZA SERIKALI MAFUTA YA KIBOKO


Na  Walter  Mguluchuma
Katavi
Mtu mmoja  Mkazi wa  Mtaa wa Kawajense Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi  amekamatwa akiwa na Nyara  za Serikali mafuta ya mnyama Kiboko   kufutia msako mkali uliofanywa na Askari wa Jeshi la polisi na TANAPA
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari  alimtaja mtuhumiwa huyo aliyekamatwa na Nyara za Serikali mafuta ya Kiboko kuwa ni  Mashaka George (32) Mtaa wa Kawajense
Kidavashari aliwaambia waandishi wa habari kuwa  mtuhumiwa  huyo alikamatwa  hapo juzi  majira ya saa  tisa na nusu alasiri   huko  katika Kijiji cha  Kisilami  Kata ya Ugala  Wilaya ya Mlele
 Alieleza  mtuhumiwa alikamatwa kufutia taarifa zilizotolewa  kutoka kwa Raia wema  kwa   Jeshi la Polisi na  Askari wa   TANAPA kuwa mtuhumiwa  George  amekuwa akijihusisha na uwindaji haramu
Baada ya taarifa hizo zilizotolewa na Raia wema wanaoishi Kijijini hapo   polisi kwa kushirikiana na TANAPA walikwenda kijijini hapo kwa lengo la  kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo
 Kamanda wa Polisi   Kidavashari alisema  baada ya kufika  kwenye Kijiji hicho  Askari Polisi na askari wa TANAPA walifanya msako wa kumsaka mtuhumiwa na ndipo walipoweza kumkamata huku akiwa na mafuta ya mnyama Kiboko zaidi ya lita moja na nusu akiwa ameyahifadhi kwenye chupa
Mtuhumiwa  anaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote mara baada ya uchunguzi wa tukio hilo utakapo kuwa umekamilika
 Alifafanua  mafanikio  ya kukamatwa kwa watuhumiwa mbalimbali ambao wamekuwa wakijihusisha na uwindaji haramu  katika   Hifadhi ya Taifa ya Katavi na nje ya hifadhi  umetokana na ushirikiano mkubwa  na mzuri  uliopo  kati ya jeshi la polisi ,Askari  wa wanyama pori wa TANAPA  na raia wema  ambapo wamekuwa wakiendelea  kutoa taarifa  za uharifu  na kufanikisha katika ukamataji

    
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

No comments:

Post a Comment