Tuesday, August 7, 2012

WAUZA MATUNDA WAWAGOMEA POLISI

Walter Mguluchuma, Mpanda
WAFANYABIASHARA wa matunda katika soko kuu la mji wa Mpanda wamewatunishia misuli askari wa jeshi la polisi waliokuwa wakiwataka wafanyabiashara hao wasishushie matunda yao katika eneo la soko.
Tukio hili limetokea jana majira ya saa 10:30 jioni baada ya gari aina ya Scania kufika katika eneo la soko kuu likiwa limetokea wilayani Kasulu, mkoa wa Kigoma, huku likiwa limepakia mananasi, ndizi na mapalachichi.
Baada ya gari hilo kufika katika eneo hilo askari wa usalama barabarani wakiwa na askari wa kawaida waliwataka wafanyabiashara wasitelemshe matunda katika eneo hilo la soko na badala yake wakapakulie katika eneo la soko la Kawajense.
Kufuatia maelekezo hayo wafanyabiashara waliwakatalia askari hao na kuwaeleza kuwa wao hawako tayari kwenda kupakua mizigo yao huko kwa madai kuwa eneo hilo halifai kwani halina huduma muhimu za choo na miundombinu mingine.
Pamoja na maelezo hayo, polisi waliendelea kuwataka wasishushie katika eneo hilo na kusababisha mzozo mkali kati yao huku wauza matunda wakipaza sauti kwamba wako tayari kuuawa kuliko kuondoka eneo hilo.
Wauza madunda hao waliamua kushusha matunda hayo na kuwaacha polisi wakiwa wameduwaa wasijue la kufanya.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mpanda Ferdinand Filimbi alisema halmashauri yake kwa sasa haina fedha za kuwekea miundombinu kwenye soko hilo la Kawajense.
Blogzamikoa

No comments:

Post a Comment