MKUU wa mkoa wa Katavi, Dr Rajabu Rutengwe amewataka wawekezaji wanaokwenda kuwekeza katika sekta ya madini katika mkoa wa Katavi wawasiliane na ofisi za serikali mkoani humo kabla ya kuingia katika mikataba ya uendeshaji wa shughuli za uzalishaji katika maeneo husika
Mwandishi wa habari hii kutoka Katavi Willy Sumia anaripoti kuwa wito huo umetolewa na mkuu kufuatia utapeli waliofanyiwa wawekezaji wa kutoka nchi ya China na kampuni yao ya Red Ore Mining Co. Ltd ya DSM na kupelekwa eneo la pori la akiba la Luafi mpakani na hifadhi ya Taifa ya Katavi kwa ajili ya kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini ya chuma na shaba.
Taarifa zinasema kuwa kampuni hiyo yenye makao yake jijini DSM inayoendeshwa na Raia wa nchi ya China ilianza shughuli katika eneo hilo katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita hadi jana walipofika askari wa wanyamapori wa Pori la akiba la Rukwa / Lukwati/ Luafi na hifadhi ya Taifa ya Katavi kuwaamuru waondoke katika eneo hilo kwakuwa ni eneo lilitengwa kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira na ustawi wa wanyama pori.
Askari hao walipozungumza na waandishi wa habari walisema kuwa awali walipowakuta raia hao wa China waliweza kuwahoji na kubaini kuwa walikuwa wameingizwa eneo hilo kimakosa na ofisi ya hifadhi hiyo iliwaandikia barua yenye Kumb Namba RLLGR/LGR.1/72/14 ya tarehe 06/06/2012 iliyokuwa akiwapa amri ya kuondoka eneo ndani ya siku saba tangu tarehe ya barua hiyo lakini hawakuweza kutekeleza agizo hilo
Askari hao wa wanyamapori walisema kutokana na kushindwa kutii agizo hilo waliamua kufika eneo husika kuwachukua viongozi wa kampuni hadi ofisi ya Mkuu wa mkoa kwa maamuzi zaidi kwani walibaini kuwa walipewa taarifa za uongo na mtu aliyewauzia hilo eneo kwani hilo eneo na eneo lisilotakiwa kufanyiwa shughuli yoyote ile
Walisema hata barua walizojibiwa na Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii yenye kumbukumbu namba HB 178/286/01/102 iliyosainiwa na ndugu J. Muya kwa niaba ya Katibu mkuu wa wizara hiyo ya tarehe 20/06/2012 pamoja na ile iliyotoka kwa wakala wa misitu Tanzania (TFS) yenye kumbukumbu namba TFSC.166/286/01/29 ya tarehe 25 Juni, 2012 ikieleza kuwa eneo hilo waliloomba kwa barua siyo eneo linaloruhusiwa kwa kufanya shughli yoyote ya kibinadamu isipokuwa kwa utafiti wa mafuta, gesi au madini ya uraniamu tu
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao na Wachina wamiliki wa Kampuni ya RedOre Mining Co. Ltd, mkuu wa mkoa wa Katavi, Dr Rajabu Rutengwe alisema kuwa katika mazungumzo na wawekezaji hao alibaini kuwa walitapeliwa na mtu aliyewauzia eneo hilo baada ya kuona kuwa eneo hilo haliruhusiwi kwa shuguli yoyote.
Alisema kutokana na hali iliyojitokeza inabidi sheria ichukue mkondo wake na huku wawekezaji hao wakiwa nje ya hifadhi kwani tayari eneo hilo limeshaharibiwa na kuingiza hasara kubwa Taifa hivyo ili kuepusha malalamiko ya kuwa wageni hao wameonewa na Watanzania hivyo mahakama ndiyo itakayoamua nani kakosea, wapi na namna gani kakosea ili kulinda utawala bora.
Akizungumzia juu ya aliyewatapeli wawekezaji hao mkuu wa mkoa alisema wao ndio wanamfahamu aliyewauzia na wanafahamu watampata wapi hivyo ni jukumu la wawekezaji kumtafuta wamuawajibishe kwa kuwatapeli ambapo mkuu huyo wa mkoa alitoa ushauri kwa wawekezaji wengine wasiingie mkataba na mmiliki yeyote wa ardhi katika mkoa wa Katavi bila kuwasiliana na Halmashauri au ofisi ya madini ya kanda ya Magharibi iliyoko mjini Mpanda kwa ushauri na msaada wa taarifa za eneo husika.
No comments:
Post a Comment