Monday, May 30, 2016

MIAKA 12 JELA KWA KUJIFANYA YEYE NI AFISA JESHI LA POLISI NA KUTAPELI FEDHA KIASI CHA TSH 800,000

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Na  Walter   Mguluchuma
Katavi

MAHAKAMA ya  Wilaya  ya  Mpanda  Mkoa wa   Katavi  imewahukumu   Alex  Chotala(24) pamoja  na  Gabriel  Katabi (25) wote wakazi wa mji wa Mpanda kifungo  cha  miaka  12  jela  baada  ya kupatikana  na   kosa  la kujifanya   maafisa wa  jeshi la  Polisi na  kutapeli  fedha kiasi  cha  shilingi 800,000.

Hukumu  hiyo  ilitolewa Mei 27  na  Hakimu   Mkazi  wa  Mahakama ya  Wilaya ya  Mpanda Odira  Amworo  baada ya  Mahakama  hiyo  kuridhika  na   ushahidi  uliotolewa  mahakamani   hapo .

Awali  katika   kesi  hiyo   Mwanasheria  wa  Serikali Mkoa  wa   Katavi  Malifimbo  Hongera  alidai  mahakamani  kuwa  washitakiwa  walitenda  kosa  hilo Agosti 31    mwaka  jana katika   Kijiji  cha   Kapanga  Tarafa ya  Mwese  Wilayani  humo.

 Alidai kuwa washitakiwa walijitambulisha  kwa     msichana  aitwaye   Vishiti   Mkono(21)   mkazi wa Kijiji  cha   Kapanga  kuwa  wao  ni  maafisa wa  jeshi  la  Polisi  Wilaya  ya   Mpanda na kutokana na vyeo walivyo navyo  wanauwezo wa kumsaidia kujiunga  na  Jeshi la  Kujenga   Taifa  JKT hivyo walimtaka   afike   katika  kituo  cha polisi cha  Mpanda  Mjini  akiwa na  cheti  cha  kuzaliwa na vya kumalizia  shule  na walimpatia  namba za simu ili  akifika awapigie.

Malifimbo  aliieleza  Mahakama   Vishiti alifanya  kama  ambavyo  alivyoelekezwa  na  washitakiwa na siku waliyokubaliana alipofika aliwapigia  simu  washitakiwa  ambao walimtaka  wamkute  nyuma  ya  jengo  la kituo  cha  polisi  cha   Mpanda   mjini kwa kile walichodai  ofisini kwao kulikuwa na kikao kinaendelea  cha  maafisa  wa  polisi.

 Washitakiwa  hao  walifika    nyuma  ya  jengo  hilo na kumtaka  awapatie  vyeti walivyokuwa wamemuagiza  na  baada ya  kuwapatia walimweleza Dada  huyo awapatie  kiasi cha Tsh  800,000 kwa kuwa   cheti  chake  chake  ni  cha  darasa  la  saba ili  fedha  hizo wakawapatie  maafisa  wenzao  wa  jeshi  la  Wananchi  ambao  wanahusika  na  usaili.

Vishiti  alifanya  hivyo  na  ndipo  walipomchukua  na kwenda  nae   eneo  la  Ofisi  ya  Mkuu wa  Wilaya  ya  Mpanda kwa  lengo  la kupeleka  vyeti   na  walimuacha  hapo   barabarani kwa zaidi ya saa nne kisha walirudi na  kumwambia  kuwa  vyeti  vyake  vimepokelewa  na kukubaliwa.

Baada ya kupeleka vyeti hivyo na fedha mtuhumiwa Katabi alifuatana na msichana huyo mpaka katika nyumba ya kulala wageni ambapo walilala wote na kisha kushirikiana kimapenzi kwa madai kuwa atafanya kila liwezekanalo hadi apate nafasi ya kujiunga na jeshi hilo.

Mwanasheria  huyo  alieleza  siku  iliyofuata  Dada  huyo  alirudi  Kijijini kwao  Kapanga  ambako  alikuwa  akifanya  kazi  ya kuuza  duka  la  dawa  za   Binadamu wakati  akiwa  anasubiri  muda ufike wa kwenda kujiunga  na  jeshi la kujenga Taifa .

Baada ya  wiki  moja   washitakiwa  walimtumia barua  ambayo ilikuwa ni yakughushi ikiwa  inaeleza  kuwa  amechaguliwa  kujiunga  na  jeshi la  kujenga  Taifa    Itende  Mbeya   barua  ambayo  ilitolewa  mahakamani  hapo kama  kielelezo .

Hakimu     Mkazi   Odira   Amworo  kabla ya  kusoma  aliiambia  Mahakama  kuwa  washitakiwa  wote wawili  wamepatikana  na  hatia  ya  makosa  manne  kati ya   matano waliokuwa wameshitaki   hivyo  kama  wanayosababu ya  msingi ya kuweza kuishawishi  Mahakama  iwapunguzie  adhabu wanapewa  nafasi ya kujitetea.

Washitakiwa  katika  utetezi wao  waliiomba  Mahakama  iwapunguzie  adhabu kwa kuwa  umri wao  bado  ni  mdogo    na wanatarajia kuoa  hivi  karibuni .

Akisoma  hukumu  hiyo  Hakimu  alielez Amworo katika  kosa la kwanza la kujifanya  maafisa wajeshi la  Polisi  Mahakama  imewahukumu  kifungo cha  miaka  mitatu jela ,Kosa  la  Pili  la kufoji  barua  kifungo  cha  miaka mitatu,kosa  tatu kujipatia  fedha kwa njia ya udanganyifu  kifungo  cha  miaka  mitatu  na kosa  la  nne  kujifanya  matapeli  kifungo  cha  miaka  mitatu.na kosa la tano la kufanya mapenzi kwa njia ya ulaghai waliweza kuondolewa kwa kukosekana  ushahidi wa  kutosha

Hakimu huyo alisema makosa  hayo  yote  adhabu yake  inakwenda  pamoja  hivyo washitakiwa  watatumikia  kifungo  cha  miaka  mitatu  jela  kuanzia  juzi na kulipa  fedha  Tsh  800,000 walizotapeli ili arudishiwe aliyetapeliwa
 

No comments:

Post a Comment