Sunday, September 7, 2014

Watendaji wa Serikali 18 watimuliwa kazi Nkasi

  Walter  Mguluchuma Mpanda

WAKULIMA wadogo mkoani Rukwa, wameshauriwa kujiunga na vyama vya wakulima (AMCOS) ili viweze kuwasaidia kupata pembejeo za kilimo na masoko mara baada ya kuzalisha mazao yao.

Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Rukwa, Wallace Kiama alisema hayo jana wakati akikabidhi cheti cha utambulisho kwa chama cha ushirika wa wakulima cha Muzia (AMCOS) mara baada ya chama hicho kupata viongozi wapya.
Alisema kuwa iwapo wakulima watajiunga na AMCOS ni wazi wataweza kusaidiwa kupata pembejeo za kilimo kwa gharama nafuu tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi wao wananunua kwa bei kubwa kiasi kwamba wengine wanashindwa kumudu.

Kiama aliongeza kuwa faida nyingine ya kujiunga na ushirika huo unasaidia kuhakikisha linakuwepo soko la uhakika la bidhaa zao walizozalisha ukizingatia kwamba hivi sasa kumekuwepo na uzalishaji mkubwa wa mahindi lakini hakuna soko la uhakika kwani NFRA inayonunua mahindi kwa ajili ya Serikali imeweka kipaumbele kwa vyama vya wakulima na wafanyabiashara wadogo.

Katika uchaguzi  huo, Muzia AMCOS ailipata viongozi wapya ambapo Linus Patrick alichaguliwa kuwa mwenyekiti, wakati nafasi ya makamu mwenyekiti alichaguliwa Lucas Msangazila ambapo viongozi hao wataidiwa na wajumbe nane wa bodi ya chama hicho waliochaguliwa.
Awali msimamizi wa uchaguzi huo, afisa ushirika Lema Emmanuel aliwataka wajumbe kuchagua viongozi wenye weredi na watakaoweza kukisaidia chama hicho kupata maendeleo endelevu na kufikia malengo yake ya kukuza kipato cha mtu mmoja kupitia kilimo.

Aliwataka viongozi hao kuepuka migogoro isiyo na tija kwani mara kadhaa mifarakano hiyo imesababisha vyama vingi vya ushirika kufa na mkulima kukosa mkombozi.

Mwisho.

Walter Mguluchuma  Mpanda
MADIWANI wa halmashauri ya wilaya Nkasi mkoani Rukwa wamewatimua kazi watendaji 18 wa halmashauri hiyo na wengine wawili wakipunguziwa mishahara baada ya kukutwa na makosa kadhaa.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri Kimulika Galikunga alisema jana kwamba madiwani wamefikia hatua ya kuwafukuza kazi watumishi hao baada ya kuridhishwa na taarifa za tume mbalimbali zilizokuwa zinawafuatilia  watumishi hao na kufikia hatua hiyo ya kuwafukuza kazi.

Alisema kuwa watumishi hao wamefukuzwa kwa makosa makubwa mawili ambayo ni ya kukusanya fedha kwa wananchi na kuzitumia kinyume cha utaratibu ikiwa ni pamoja na wengine kuwa watoro kazini kwa muda mrefu.

Alisema kuwa watumishi waliofukuzwa kuwa ni maofisa watendaji wa vijiji 7 ambapo kati yao wawili wamepewa adhabu ya kupunguziwa mshahara, pia wao wauguzi wa hospitali na Maafisa kilimo wasaidizi.

Mkurugenzi huyo alidai kuwa watumishi hao wamekumbwa na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma na wengine kwa utoro wa muda mrefu kazini na baada ya uchunguzi wa kina makosa yao yamebainika na kuwa suluhisho imekuwa ni kuwafukuza kazi watumishi hao.

Pia katika kikao hicho, madiwani wa halmashauri hiyo waliwataka watendaji wa halmashauri hiyo kujipima sawasawa kama wana uwezo wa kufanya kazi na kama hawana uwezo huo basi wawapishe kabla wao hawajachukua hatua.

Akichangia katika kikao hicho mara baada ya kupata ripoti ya mkaguzi mkuu mkazi na mdhibiti wa fedha za serikali mkoani Rukwa John Nalwanda diwani wa kata ya Nkomolo Sospeter Kasawanga alidai kuwa ripoti ya mkaguzi huyo ni nzuri na inaonyesha wao kupata hati safi katika kipindi cha mwaka 2012-13 na kuwa hawataki tena kuona kuwa wanapata hati chafu au yenye mashaka.

Alisema ni muda mrefu sasa halmashauri hiyo imekua ikipata hati zenye mashaka na kumpongeza mkurugenzi mtendaji wa sasa Kimulika Galikunga kwa utendaji wake mzuri na kumtaka kuendelea  kuwasimamia watendaji wake hao ili waweze kufanya vizuri zaidi na kuwa kwa kufanya hivyo wananchi ndiyo wanaonufaika kutokana na huduma za serikali kuimarika.

Diwani wa kata ya Kipili Kapunda Mbwilo aliwataka watendaji hao kukaza uzi kutokana na taarifa nzuri ya mkaguzi na mdhibiti wa fedha za serikali na kumtaka mkurugenzi kuendeleza moto wa kuwabana watendaji wake na kuwa wao kamwe hawatasita kumwajibisha mtu yeyote atakayekwenda kinyume na maadili ya kazi.

Mkuu wa wilaya Nkasi Idd Hassan Kimanta kwa upande wake  aliwataka watendaji hao kuzidisha mshikamano miongoni mwao na mkurugenzi wao na kuwa siri ya mafanikio ni umoja na kuwa yeye kama kiongozi wa serikali hatamvumilia mtu atakaepelekea halmashauri hiyo kudorora na kuharibu sifa nzuri waliyoijenga sasa ya kupata hati safi


Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

No comments:

Post a Comment