Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SHIRIKA
la Hifadhi za Taifa (TANAPA), limekanusha taarifa zinazodai Hifadhi ya
Taifa ya Katavi ipo kwenye mpango wa kukabidhiwa kwa wawekezaji kutoka
nchini Afrika Kusini.
Habari hiyo iliandikwa Machi 25 mwaka huu na
gazeti moja linalotoka mara moja kwa wiki ikiwa na kichwa cha habari
kinachosema, "Nyalandu 'auza' Hifadhi”.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na TANAPA kupitia Idara yake ya Mawasiliano, ilisema habari
hiyo ilidai agizo la hifadhi hiyo kupewa wawekezaji, limetolewa na
Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu
Idara hiyo
imeongeza kuwa, TANAPA ambayo ndio wasimamizi wa hifadhi hiyo na
nyingine 15 nchi nzima, inakanusha habari hiyo na kudai imeandikwa kwa
lengo la kupotosha umma.
"Hakuna mpango wala uamuzi wowote uliopo au
uliofanywa wa kuingia mkataba wa uendeshaji hifadhi yoyote nchini kati
ya TANAPA na mwekezaji yeyote kutoka nchini humo wala African Parks
Network waliotajwa katika habari husika.
"Sheria inayosimamia
uanzishwaji maeneo ya Hifadhi za Taifa ikiwemo Katavi, imelipa dhamana
shirika kusimamia maeneo haya kwa niaba ya Watanzania hivyo ni kinyume
cha sheria kukabidhi kwa wawekezaji kwa ajili ya usimamizi kama
ilivyobainishwa katika habari hiyo," ilisema taarifa ya idara hiyo.
Iliongeza
kuwa, TANAPA bado lina uwezo thabiti wa kusimamia uendeshaji wa hifadhi
hiyo ili kuhakikisha rasilimali za wanyama na mimea zinaendelea
kutunzwa kwa miaka mingi ijayo kama ambavyo imekuwa ikifanya tangu
kuanzishwa kwa hifadhi husika 1974.
Taarifa hiyo ilisema shirika
hilo limekuwa na mipango yake ya maendeleo mwaka hadi mwaka ambapo
katika mwaka mpya wa fedha ujao, limepanga kuongeza idadi ya watalii
katika Hifadhi za Kusini ikiwemo Katavi, Saadani, Mikumi na Ruaha.
Mkakati
huo utahusisha kuongeza ubora wa utoaji huduma na malazi ili kukuza
utalii wa ndani ambapo TANAPA itafungua ofisi jijini Dar es Salaam,
kuimarisha Ofisi za Mwanza na Iringa ili watalii wapate taarifa za
hifadhi.
"Shirika litaendelea kujitangaza kupitia mitandao ya jamii,
majarida, televisheni na kuiboresha tovuti ya shirika kwa kuwarifu
wadau masuala mbalimbali yanayojiri kwenye hifadhi zetu.
"Tayari
Shirika limeanzisha Kurugenzi mpya ya Utalii na Masoko kwa ajili ya
kutekeleza mkakati wa kuzifanya hifadhi za Ukanda wa Kusini kuvutia
watalii wengi zaidi," alisema.
Chanzo;Majira
No comments:
Post a Comment