Saturday, September 8, 2012

WAOMBA KUPATIWA ELIMU YA KUTENGENEZA MAJIKO SANIFU.

Mussa Mwangoka, Katavi Yetu

WANAWAKE wa Kata za Katuma na Nsimbo wilayani Mpanda mkoa wa Katavi wameiomba Serikali na wadau wa Mazingira kuwapatia elimu ya namna ya kutengeneza majiko banifu na sanifu ambayo  yanatumia nishati kidogo ya mkaa ili kupunguza kasi ya ukataji miti na uchomaji wa misitu ovyo.

Hayo yameelezwa kwa nyakati tofauti wakati wa midahalo iliyolenga kuwaelimisha kuhusu mabadiliko ya tabianchi, iliyoandaliwa na muungano wa asasi isiyo ya kiserikali mkoani Rukwa (Rango) kwa ufadhili wa shirika la Civil Society For Foundation.

Mmoja wa wanawake hao Maria Kaseya alisema kuwa iwapo watapata elimu ya matumizi ya teknolojia hiyo yatasaidia kuzuia uharibifu wa mazingira na kupunguza magonjwa ya mapafu kwa binadamu.

Alisema wakati umefika kwa wananchi kubadilika kutoka kutumia majiko ya kizamani na kutumia majiko mapya ambayo yanayotumia teknolojia yenye kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa pamoja na kupunguza matumizi ya kuni na miti

Naye Elizabeth Msafiri aliongeza kuwa iwapo Serikali na wadau wengine watajikita katika kutoa elimu hiyo itakuwa ni njia moja wapo ya kupunguza kasi ya uharibifu wa mazingira iliyopo hivi sasa.
.
Alisema kuwa taasisi nyingi zisizo za kiserikali zimekuwa zikitoa elimu hiyo kwenye maeneo mengine hivyo sasa ni muhimu na wao wakapata fursa ya kuelimishwa kuhusu utengenezaji majiko yanayoelezwa ni chachu ya kupunguza uharibifu wa mazingira nchini.

Mmoja wa wawezeshaji katika mdahalo huo, Tumaini Suleiman alisema chanzo kikuu cha mabadiliko ya Tabianchi ni kuongezeka kwa joto duniani, kunakosababishwa na gesijoto kwa kiwango kikubwa kuliko kiasi halisi kinachohitajika kuwezesha uhai na mifumo ya dunia kuwa katika hali yake ya asili.

Aliongeza kuwa katika mazingira yetu, gesijoto ni Carbon-Dioxide, Methani na nyinginezo ambazo zinatokana na shughuli za kila siku za Mwanadamu, kama vile viwanda, vyombo vya usafirishaji, ukataji misitu, uchomaji moto ovyo pamoja na kilimo kisicho endelevu.

Suleiman aliongeza kuwa athari za mabadiliko ya Tabianchi zinazoweza kutukabili tusipochukua tahadhari ambazo ni kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuhifadhi mazingira.
Blogzamikoa

No comments:

Post a Comment