Home » » MAKALA MUHIMU: NYUMBA YA MKUU WA SHULE YA MSINGI YA MTAPENDA HAINA CHOO.

MAKALA MUHIMU: NYUMBA YA MKUU WA SHULE YA MSINGI YA MTAPENDA HAINA CHOO.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.





*Ni katika shule yenye umri wa zaidi ya miaka 40
*Tatizo la maji ya kujisitiri msalani lazidisha kero
NA WALTER MGULUCHUMA, Katavi
Wakati Bunge la Bajeti likiendelea na vikao vyake mjini Dodoma, wadau wa elimu mkoani Katavi wameonekana kusikitishwa na uduni wa mazingira yaliyopo katika shule mbalimbali mkoani hapa.
Katavi ni miongoni mwa mikoa inayofanya vyema katika sekta ya elimu kwa miaka ya karibuni, ikishika nafasi za juu katika matokeo ya jumla ya darasa la saba na hata kidato cha nne.
Lakini nyuma ya mafanikio hayo yanayodaiwa kupatikana kwa jasho la walimu wenye uzalendo mkubwa na kitihada za wazazi na wanafunzi, shule nyingi zimekuwa zikikabiliwa na mazingira duni katika kila hali.

Utafiti uliofanywa na  MWANDISHI WA HABARI HIZI uligundua kuwa moja kati ya shule zenye changamoto zinazoweza kutatuliwa kwa ushirikishwaji kati ya serikali na wadau ni Shule ya Msingi Mtapenda.
Shule hiyo ipo katika Halmashauri ya Nsimbo, Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, ikiwa takriban kilomita 15 tu kutoka mkoani, lakini haina makazi ya walimu na nyumba iliyopo inayotumiwa na Mwalimu Mkuu, haina hata choo.
Shule hiyo ilianzishwa zaidi ya miaka 40 iliyopita wakati Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ilipoendesha Operesheni Vijiji.
Walimu 16 wanaofanya kazi shuleni hapo kwa sasa wote wanaishi katika nyumba za kupanga, nyingi zikikosa hadhi ya kuishi mfanyakazi wa serikali na hivyo wengine kuishi kijiji jirani, wakilazimika kusafiri mwendo mrefu kufika kazini.
“Hata hiyo nyumba anayoishi Mwalimu Mkuu nayo ni majanga tu. Haina choo! Kwa hiyo mwalimu analazimika kuomba msaada kwa majirani kujisitiri. Ni aibu kwa kweli,” anasema mmoja wa walimu wa shule hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Hata hivyo, zipo nyumba (au tuseme mahame) zilizokuwa zimejengwa kwa ajili ya walimu jirani na shule hiyo ambazo kwa hakika ni chakavu kiasi cha kuonekana kama ‘makaburi’ kwa yeyote atakayejaribu kuzitumia, zikiwa zimejengwa kwa udongo.
Mwalimu mmoja aliyejitosa kuishi katika moja ya nyumba hizo anadai kuwa nyakati za mvua huwa hakuna kulala kwani nyumba hizo zinavuja.
“Ni sawa na kukaa chini ya mwembe. Hapo utafurahia kivuli tu lakini mvua ikija, hapafai,” anasema mwalimu huyo.
 Diwani wa Mtapemba, Eliezer Fyula anakiri kulifahamu tatizo la uhaba wa nyumba shuleni hapo, akidai kuwa lipo kwa muda mrefu sasa.
“Hapa tuna bahati kwa kuwa tuna walimu 16, lakini ni bahati mbaya kwamba nyumba zilizoandaliwa kwa ajili yao ni tano tu, nazo ni chakavu kama unavyoziona.
“Ni moja tu ndio imejengwa kwa matofali ya kuchoma, nyingine ni matofali ya udongo tu. Wenyewe wanaita biskuti. Zipo katika hali mbaya sana,” anasema Fyula.
Anasema tatizo hilo linachagizwa na Halmashauri ya Nsimbo kutotenga fedha kwa ajiri ya ujenzi wa nyumba za walimu licha ya yeye kuishauri mara kwa mara.
Kwa upande mwingine, katika Kijiji cha Majimoto wilayani Mlele, tatizo la maji lililopo maeneo hayo husababisha hata wanafunzi kushindwa kuendelea na ratiba ya masomo kama ilivyopangwa.

Katika Shule ya Msingi Majimoto,  MWANDISHI WA  HABARI HIZI  iliwashuhudia watoto wakitoka madarasani kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi, hasa ya chooni, kwani shule haina kisima wala bomba la maji.
Wakizungumza na mwandishi wetu, wanafunzi hao waliokuwa wakichota maji katika chemchem maarufu inayotoa maji ya moto, walilalamikia hali hiyo.
“Shuleni hakuna huduma yoyote ya maji na kama kusingekuwapo chemchem hapa karibu, sijui tungepata wapoi maji. Kila mara huwa tunakatisha masomo kuja kuchota maji,” anasema mtoto mmoja wa darasa la tatu.
Ni kawaida kwa kila mwanafunzi anayesoma shuleni hapo kuwa na dumu (kopo la plastiki) la lita tano kwa ajili ya kuchotea maji kwenye chemchem hiyo.
Jina la kijiji, Majimoto, linatokana na kuwapo kwa chemchem hiyo inayotoa maji ya moto kiasi cha kulazimika kuyapoozesha kabla ya kuyatumia. Maji hayo hutiririka kwa mwaka mzima.
Hata hivyo, maji hayo yanayotokana na nguvu za asili (volcano), hayafai kwa kunywa.
“Tumeshazoea kwa sababu imekuwa kawaida kabisa kuja kuchota maji hapa. Tutfanyaje na chooni hakuna maji? Ni lazima kila sku kuja hapa kuchota maji,” anasema binti huyo.

Pamoja na kufahamu kwamba maji ya chemchem hiyo hayafai kwa kunywa, MWANDISHI iliwashuhudia watoto kadhaa wakiyanywa baada ya kupoa, wakisema hawana sehemu nyingine ya kupata maji ya kunywa.
Kwa ujumla maji ni tatizo kubwa kijijini hapo na wananchi husafiri kwa takriban kilomita sita kufuata maji katika Kijiji cha Mamba.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Katavi yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa