Na Walter Mguluchuma .
Katavi .
Makamu wa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda Padri Patrick Kasomo amewataka watu waache tabia ya kuzaa watoto wengi na badala yake wazae watoto ambao wataweza kuwatunza kwa kuwapatia mahitaji yao ya muhimu.
Wito huo aliutowa hapo jana wakati wa mafunzo ya viongozi mbalimbali wa Dini wa Kanisa hilo yaliondaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation na yaliofanyika katika ukumbi wa Chekechea Mjini hapa yaliokuwa na lengo la kuwaelimisha watu kujikinga na kujiepusha na Ukimwi.
Alisema watu watu wamekuwa na tabia ya kuzaa watoto wengi bila mpangilio na matokeo yake wakuwa wakishindwa kuwatunza watoto hao kutokana na kuwa na uchumi mdogo wa kipato .
Makamu huyo wa Askofu alieleza familia nyingi za watu maskini ndio zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya kuzaa watoto wengi kuliko watu wenye uwezo wa kiuchumi .
Alisema watu ambao wanazaa watoto wengi matokeo yake watoto hao wanakuwa hawana akiri darasani hivyo ni vema watu wakazaa watoto ambao wanaweza kuwatunza .
Pia aliwataka watu wajenge tabia ya kupima afya zao na wawe waaminifu kwenye ndoa zao na wasiige utamaduni wa Nchi nyingine ambao umekuwa ni chanzo cha wtu kuacha kufuata mila na utamaduni wa Nchi yetu .
Afisa mradi wa TB na HIV wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Magiri David alisema Taasisi ya Benjamin Wiliam Mkapa kupitia Save the Children imepokea ufadhili kutoka mfuko wa Dunia wa kupambana na maambukizi ya kifua kikuu TB ,virusi vya ukimwi VVU na Malaria ambao utatekelezwa kwa muda wa miaka miwili.
Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya , Maendeleo ya jamii Jinsia Wazee na Watoto kupitia mpango wa Taifa wa kuratibu huduma za UKIMWI umetowa mafunzo hayo kwa viongozi wa dini ya kuhusu elimu juu ya maambukizi ya Ukimwi.
Magiri alisema baada ya kupatiwa elimu hiyo viongozi hao wa Dini wanategemewa kuwa watakuwa mabalozi wazuri katika jamii kwa kuweza kufikisha elimu walioipata kwa jamii inayowazunguka ili kupunguza maambukizi ya VVU na pia wao wenyewe kujikinga na maambukizi ya VVU .
Mafunzo hayo yatatolewa katika Mikoa ya Tabora na Rukwa na yatawafikia waumini wa madhehebu ya Dini mbalimbali wasiopungua 500 hadi kufikia Desemba mwaka huu.
Nae mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Benjamin Mkapa Foundation Peter Nyambo alieleza kuwa umefika wakati sasa kwa watoto wadogo kuelimishwa ili waache kufanya tendo la ndoo wakati wakiwa na umri mdogo .
Tabia ya watoto kuanza kufanya tendo la ndoo kumekuwa kukichangia watoto hao kupata maambukizi ya VVU kutokana na kutojua kujikinga na maambukizi ya VVU.
Alisema Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation imeamua kuwapatia mafunzo viongozi wa madhehebu mbailimbali ya Dini ili na wao waende wakatowe elimu kwenye makundi mbalimbali juu ya kujikinga na maambukizi ya VVU .
Alifafanua kuwa Taasisi hiyo imepanga kuendelea kutowa elimu iliifikapo mwaka 2030 maambukizi ya VVU yawe yamekwisha kabisa hapa Nchini Tanzania .
Mratibu wa Ukimwi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Kasara Bulemo alisema Wamejipanga kufika kwenye Kata zote 16 za Halmashauri hiyo ili kutowa elimu ya kupima maambukizi ya VVU kwa hiari .
Alisema maambukizi ya VVU katika Mkoa wa Katavi ni 5.9 na yamekuwa yakichangiwa sana kwenye maeneo ya mikusanyiko ya watu hasa wakati wa msimu wa mavuno .
Aliyataja baadhi ya maeneo yenye maambukizi mengi ya VVU katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda kuwa ni Karema , Ikola , Mnyagala na Kasekese.
0 comments:
Post a Comment