Home » » WAZIRI MKUU MH.PINDA AWATAKA WANANCHI KUJIANDIKISHA KATIKA DAFTARI LA KUDUMU.

WAZIRI MKUU MH.PINDA AWATAKA WANANCHI KUJIANDIKISHA KATIKA DAFTARI LA KUDUMU.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Na  Walter Mguluchuma 
Katavi
Waziri Mkuu Mizengo  Pinda amewataka wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kupata nafasi ya kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao itakapofika hapo oktoba 25 mwaka huu.
 
Waziri Mkuu Pinda ameyasema hayo juzi  mara baada ya kujiandikisha kwenye kituo cha kupigia kura ofisi ya  Mtendaji wa Kata ya Kibaoni ililiyoko Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi.
 
Amsema iwapo watajiandikisha watapata haki ya kuweza kushiriki katika uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na Madiwani unaotarajia kufanyika nchini kote.
 
“Ninawasihi Watanzania wote tusiache kutumia fursa hii ,kila mtu ahakikishe kuwa anajiandikisha, Ni fursa pekee itakayohakikisha kila mwananchi anashiriki uchaguzi wa kumpata Rais, Mbunge na Diwani,” alisema  Waziri Mkuu Pinda.
 
Waziri Mkuu alisema amefarijika kwa kazi aliyoiona ikifanyika kwani hadi sasa Halmashauri za Nsimbo na Mlele zimefanikiwa kuandikisha watu kwa zaidi ya asilimia 100.
Naye Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Taifa Julius Mallaba ameeleza kuwa hakuna mtu atakayeshindwa kuandikishwa katika zoezi linaoendelea kila aliyepo kwenye kituo lazima ataandikishwa.
 
Awali akiwasilisha taarifa ya uandikishaji katika Halmashauri ya Mlele, Mkurugenzi Mtendaji  wa Halmashauri hiyo,  Godwin Benne alisema walilenga kuandikisha watu 19,482 lakini hadi kufikia jana walifanikiwa kuandikisha watu 20,292 sawa na asilimia 105. Uandikishaji katika wilaya ya Mlele ulianza tarehe 18 Mei, mwaka huu.
 
“Mlele tuna vituo 84 katika tarafa tatu za Inyonga, Mpimbwe na Mamba. Inyonga tuna vituo 28, Mpimbwe viko 23 na Mamba viko 33.
 
Akifafanua zaidi, Bw. Benne alisema katika kata ya Kibaoni ambayo ina vituo sita, juzi peke yake walifanikiwa kuandikisha watu 1,007 kikiwemo kituo cha Kibaoni ambacho Waziri Mkuu Pinda alijiandikisha. 
 
Alivitaja vituo vingine kuwa ni Milumba, Sungusungu, Ilalangulu, Manga na Shule ya Msingi Kakuni ambako Mama Tunu Pinda alijiandikisha jana hiyo hiyo.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, uandikidhaji  katika Halmashauri ya Nsimbo uandikishaji ulianza Mei 18, 2015 kwenye kata 12 na kwamba hadi kufikia jana, kata nne zilikwishaandikisha watu 12,001 sawa na asilimia 108.9 licha ya kuwa matarajio yao yalikuwa ni kuandikisha watu 11,014. Alizitaja kata hizo kuwa ni Nsimbo, Kapalala, Magamba na Uruwira.
 
Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda hadi kufikia mwishoni mwa wiki walikuwa wameandishwa jumla ya wapiga kura 14,972 sawa na asilimia 94.6 na lengo waliweka lengo la kuandikisha wapiga kura 15,824 katika tarafa moja ya Karema walikoanzia kwenye kata za Ikola,Karema na Kapalamsenga kisha watanza kuandikisha maeneo mengine yaliyobakia ya Tarafa ya Kabungu ,Mwese.
 
Zoezi la uandikishaji  kuboresha  daftari la kudumu la wapiga kura linaendelea Mkoani Katavi na maeneo mengine nchi,ambapo wananchi Mkoani Katavi wamehamasika kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi hilo hali inaopelekea wananchi wengine kukesha kwenye vituo vya uandikishaji ili waweze kupata nafasi ya kuwahi kuandikishwa.
mwisho

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Katavi yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa